Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imeridhia kufunguliwa kwa shauri la mapitio ya mahakama kupinga uhalali wa Tume ya Rais ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Uamuzi huo umetolewa leo Alhamisi Desemba 18, 2025 na Naibu Msajili wa mahakama hiyo, Hussein Mushi, kwa niaba Jaji Hussein Mtembwa aliyesikiliza shauri hilo, kufuatia shauri la maombi ya kibali cha kufungua kesi kuipinga tume hiyo.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kuridhika kuwa waombaji hao wamekidhi vigezo vyote vitatu vya kisheria vya kustahili kupewa kibali hicho na kuwa shauri hilo lifunguliwe ndani ya siku 14, kuanzia tarehe ya uamuzi huo.
Hata hivyo, licha ya kuridhia shauri lifunguliwe, mahakama hiyo imekataa maombi ya waombaji hao kutumia kibali hicho kama amri kwa tume hiyo kusitisha shughuli zake za uchunguzi unaoendelea, mpaka pale shauri la kuipinga litakapoamuriwa.
Akisoma uamuzi huo, Naibu Msajili Mushi amesema mahakama ilikuwa na utashi wa kulikubalia au kulikataa ombi hilo, imeona kwamba kwa masilahi mapana ya umma si busara kusitisha shughuli za tume hiyo ya uchunguzi.
Shauri hilo lilifunmguliwa na watetezi wa haki za binadamu, Rosemary Mwakitwange na mawakili wawili Edward Heche na Deogratius Mahinyila, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wenzake.
Wajibu maombi wengine ni Jaji Mkuu mstaafu, Chande na wajumbe wake saba – Jaji Mkuu mstaafu, Profesa Ibrahim Juma, Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Balozi Ombeni Sefue; Radhia Msuya na Balozi Paul Meela.
Wengine ni Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu (IGP), Said Mwema, Balozi David Kapya na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa mstaafu, Stergomena Tax pamoja na Chama cha Sheria Tanganyika (TLS).
Akizungumzia uamuzi huo, mmoja wa mawakili wanaowawakilisha waombaji hao, Hekima Mwasipu amesema watafungua shauri hilo ndani ya muda uliotajwa na wataomba amri ya kusimamisha shughuli za tume hiyo.
“Tutafanya hivyo kwa hati ya dharura kuanzia leo, kwa kuwa jambo lenyewe ni la udharura, nafikiri mahakama italipa udharura uleule kama ilivyokuwa kwenye shauri la maombi ya kibali,” amesema.
Wakili wa TLS, Ferdinand Makore amesema uamuzi huo ni ushindi kwao kwa kuwa unaruhusu Watanzania kwenda kuhoji mambo ya msingi kuhusu uundwaji wa tume hiyo, hasa kama ulizingatia sheria.
“Sisi TLS tulikuwa bega kwa bega kuwaunga mkono waleta maombi baada ya kuona kwamba hiyo kesi ina masilahi zaidi ya umma kwa sababu TLS kinashughulika na masuala ya ushauri na kutetea utawala wa kisheria na kuwasaidia Watanganyika katika masuala ya kisheria,” amesema.
Tume hiyo iliundwa kuchunguza vurugu zilizosababisha uharibifu wa miundombinu na mali za umma na watu binafsi pamoja na vifo na majreuhi, kufuatia maandamano ya Oktoba 29, 2025, katika majiji na miji mbalimbali nchini.
Kufuatia matukio hayo, Novemba 18, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan aliunda tume ya kuchunguza matukio hayo na tayari imeanza kazi yake.
Wakati shauri hilo liliposilikizwa Desemba 12, 2025 mawakili wa waombaji, Mpale Mpoki akisaidiwa na Mwasipu waliieleza mahakama kuwa waombaji wamekidhi vigezo vitatu vya kupewa kibali hicho, vilivyowekwa na sheria.
Vigezo ni pamoja na hicho kinachobishaniwa, yaani kama kuna jambo au hoja yenye mgogoro inayohitaji uamuzi, maombi kufunguliwa ndani ya muda wa miezi sita tangu kutolewa uamuzi unaokusudiwa kupingwa na waombaji kuonyesha kuwa wana masilahi katika jambo hilo lenye mgogoro.
Kuhusu kigezo cha kwanza, Wakili Mpoki alieleza kwa kuangalia kiapo na kiapo kinzani ni dhahiri kuwa kuna hoja bishaniwa kwani waombaji wametoa madai na wajibu maombi wameyapinga huku wakitaka uthibitisho.
Jopo la mawakili wa Serikali lililoongozwa na Narindwa Sekimanga akisaidiwa na Daniel Nyakia na Erigh Rumisha wawakuwa na ubishi katika vigezo viwili isipokuwa uwepo wa hoja yenye mgogoro.
Rumisha alidai waombaji wameshindwa kuthibitisha kigezo hicho na kuwa kiapo cha pamoja cha waombaji kimejaa mawazo, maoni na mitizamo yao na hitimisho bila hoja za msingi.
