Manyara. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Kamani, ameonya tabia ya baadhi ya wakulima na wafugaji kuendesha shughuli za kilimo katika maeneo maalumu yaliyotengwa kisheria kwa ajili ya malisho ya mifugo.
Amesisitiza kuwa maeneo hayo ni rasilimali muhimu kwa ustawi wa sekta ya mifugo, hivyo ametoa wito kwa wadau wote kuyaheshimu na kuyatunza kwa mujibu wa sheria.
Aidha, amekumbusha kuwa ni wajibu wa watendaji wa Serikali, viongozi wa ngazi mbalimbali, pamoja na wafugaji wenyewe kuhakikisha wanalinda maeneo ya malisho badala ya kuwa mstari wa mbele katika kuyakiuka, jambo ambalo husababisha migogoro ya ardhi na athari kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kamani amebainisha hayo leo, wakati wa ziara yake ya kikazi alipozungumza na wananchi wengi wao wakiwa ni jamii ya wafugaji kwenye kongani za malisho katika Kijiji cha Engang’uengare, kilichopo Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, baada ya kubainika kuwepo kwa shughuli za kilimo katika maeneo hayo.
Pia, amewataka wafugaji na wakulima wanaoendeleza shughuli za kilimo katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo kuondoka mara moja, ili maeneo hayo yatumiwe kwa madhumuni yaliyokusudiwa kisheria.
Pia, Naibu Waziri ameshiriki kutoa chanjo na utambuzi wa mifugo kitaifa kwa Sayei Mussa, mmoja wa wafugaji wakubwa katika Kijiji cha Orkitikiti, na kubainisha kuwa shughuli hiyo ni endelevu.
Amesema Serikali imetenga kiasi cha Sh216 bilioni kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo kwa ajili ya utekelezaji wa chanjo na utambuzi wa mifugo kitaifa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, katika shughuli ya chanjo za kimkakati kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ng’ombe 184,673 walichanjwa dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu, mbuzi 62,746 dhidi ya ugonjwa wa sotoka, na kuku 188,197 dhidi ya ugonjwa wa kideri.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mifugo, kuimarisha afya ya wanyama, na kuchangia uchumi thabiti wa wakulima na wafugaji katika wilaya hiyo.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Remedius Mwema, akitoa taarifa ya hali ya wilaya kwa Naibu Waziri, amesema ofisi yake imekuwa ikiendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa kutenga na kuheshimu maeneo maalumu ya malisho ya mifugo kwa mujibu wa sheria na mipango ya matumizi bora ya ardhi.
Amesema elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa miongoni mwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya ardhi ili kuzuia migogoro kati ya wafugaji, wakulima, na wadau wengine wa ardhi.
Pia, kuhusu chanjo ya utambuzi wa mifugo kitaifa, Mwema amesema wilaya yake inaendelea kuunda na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuwafikia wafugaji.
Amesema juhudi hizo ni kutokana na tafiti kuonyesha kwamba bado baadhi ya wafugaji hawajafikiwa ndani ya muda unaohitajika, hivyo kuibua haja ya kuongeza mbinu za kufikia kila mfugaji ili kuhakikisha chanjo inafanikishwa kikamilifu.
