KIKOSI cha timu ya taifa, Taifa Stars kimeagwa rasmi jana kabla ya kuanza safari ya kwenda Morocco katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zinazoanza Jumapili, Tanzania ikipangwa Kundi C pamoja na Uganda, Nigeria na Tunisia.
Stars iliagwa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo pamoja na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi walioitembelea kambi ya timu hiyo iliyokuwa Cairo, Misri.
Waziri Kombo na Profesa Kabudi wameitembelea kambi hiyo juzi kabla ya kuikabidhi bendera ya Taifa, ikiwa ni ishara ya kuitakia kila la kheri na kuitia shime kuelekea kwenye kinyang’anyiro cha michuano ya Kombe la AFCON itakayoanza Jumapili hadi Januari 18 mwakani.
Akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Kombo amewasihi wachezaji wa timu hiyo kuwa ni vijana wachache kati ya wengi wa taifa hili kwa kutanguliza uzalendo kwanza na kuipigania bendera ya Taifa kwa jasho na damu ili kuliletea heshima taifa la Tanzania.
Kwa upande wa Prof. Kabudi amekiahidi kikosi hicho ushirikiano wa kila aina katika kuhakikisha kinafanya vyema katika michuano hiyo mikubwa na yenye heshima kubwa sio tu Afrika bali duniani kwa jumla.
Aidha, Prof. Kabudi amewahimiza Watanzania kuipenda na kuipa moyo timu yao ya Stars kwa kuwashangilia na wale watakaokuwa na nafasi kujiunga nao katika mechi zao zote watakazocheza huko Morocco.
Ikumbukwe Stars inashiriki fainali hizo ikiwa ni kwa mara ya nne baada ya zile za mwaka 1980 zilizofabnyikia Nigeria, 2019 pale Misri na zile zilizopita za 2023 zilizochezwa Ivory Coast na wenyeji kubeba taji inakoenda kulitetea Morocco msimu huu ukiwa ni 35 tangu fainali zilipoanzishwa 1957.
Nahodha wa Stars, Mbwana Samatta akizungumza kwa niaba ya wachezaji na timu kwa jumla amesema wanaenda Morocco kuipigania Tanzania ili kurudi na heshima kwa kutambua uwezo wa kufanya hivyo wanao na muhimu ni Watanzania kuwaombea kila la kheri.
Tanzania itaanza kukata utepe wa fainali hizo Desemba 23 dhidi ya Nigeria kabla ya kuvaana na majirani zao Uganda Desemba 27 na kumalizia mechi za makundi na Tunisia na rekodi zinaonyesha katika fainali tatu ilizoshiriki awali, timu hiyo haijawahi kushinda wala kuvuka.
