Na James K. Mwanamyoto – Arusha
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amemuelekeza Mkandarasi Mohammedi Builders Limited wa Mradi wa Ujenzi wa Stendi Kuu ya Mkoa wa Arusha, kuhakikisha mradi huo unakamilika kabla au ifikapo tarehe 30 Mei, 2026 kama ilivyoanishwa kwenye mkataba.
Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo leo Jijini Arusha, mara baada ya kutembelea mradi huo kwa ajili ya kukagua maendeleo yake na kubaini kuwa ujenzi wake umefikia asilimia 28 huku nusu ya muda wa utekelezaji wa mradi huo ukiwa umefikiwa.
“Naelekeza ifikapo Mei 30, 2026 stendi hii ya mkoa iwe imekamilika na hakutakuwa na nyongeza ya muda, mie sitegemei kusikia mkandarasi anaomba kuongezewa muda wa utekelezaji,” Prof. Shemdoe amesisitiza.
Prof. Shemdoe amesema, stendi hiyo inapaswa kukamilika kwa wakati kwani Arusha ni miongoni mwa miji ambayo itatumika kwenye mechi za Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka (AFCON) 2027, hivyo stendi hiyo itasaidia kupunguza foleni katika jiji la Arusha kutokana na ujio wa mashabiki wengi wa soka.
Aidha, Prof. Shemdoe ameelekeza wakandarasi wote wanaoteleleza miradi ya TACTIC kwenye miji 27 ambao wameomba kuongezewa muda wa kutekeleza miradi yao, wakatwe fedha kwa ajili ya kufidia hasara inayotokana na ucheleweshaji wa miradi (Liquidated damages) ili iwe fundisho kwa wakandarasi wazembe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Makala ameahidi kuwa atahakikisha maelekezo yote aliyoyatoa Prof. Shemdoe yanatekelezwa kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla, na kuongeza kuwa atasimamia kwa nguvu zake zote na weledi mkubwa ili stendi hiyo ikamilike kwa wakati.
Mradi huo wa stendi kuu ya mabasi unatekelezwa kupitia mradi wa TACTIC utakuwa na uwezo wa kubeba mabasi makubwa 41, mabasi madogo 24, taxi 22, bajaji 86 na pikipiki 129, ukiwa na thamani ya bilioni 14.3 ambao unajumuisha ujenzi wa jengo kuu la mabasi la ghorofa 2, maduka 23, maeneo ya wafanyabiashara wa chakula, nyumba ya walinzi, nyumba ya umeme na jengo la tanki la maji.



