Tanzania, Malawi kuendeleza uhusiano wa biashara ya mahindi

Malawi. Tanzania na Malawi zimeendelea kuimarisha uhusiano wa kibiashara katika zao la mahindi na kuahidi kuendelea na mshikamano ambao umedumu kwa miongo kadhaa.

Hayo yamejiri  kufuatia mazungumzo yaliyofanyika Desemba 17, 2025, jijini Lilongwe, kati ya Serikali za Tanzania, Malawi na sekta binafsi.

Katika mazungumzo hayo ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa chakula, Dk Stephen Nindi ambaye amesema Tanzania inazalisha mahindi kwa kiwango kikubwa.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na wizara hiyo leo Alhamisi Desemba 18, 2025, Dk Nindi amesema Tanzania inazalisha mahindi ya kutosha na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ina akiba ya zaidi ya tani 500,000 za mahindi, hivyo Tanzania iko tayari kuendeleza uhusiano wa kibiashara na Malawi kulingana na mahitaji.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Malawi, Erica Maganga amesema nchi hizo zinaendelea kuwa na uhusiano wa karibu wa kindugu.

Maganga amesema mazungumzo hayo yanalenga kutoa fursa za kuimarisha biashara ya mahindi na ushirikiano wa kukabiliana na changamoto za usalama wa chakula unaochangiwa na mabadiliko ya tabianchi.

Ujumbe huo wa Tanzania ulikutana na uongozi wa NFRA Malawi na uongozi wa Chama cha Wauzaji na Wasindikaji wa Nafaka cha Malawi (GTPA), walijadili fursa za kibiashara za zao la mahindi, masuala ya udhibiti wa sumukuvu na changamoto za masoko.