Tusa yafunguliwa UDOM, vyuo vyahimizwa kuwekeza katika michezo

Taasisi za elimu ya juu zimetakiwa kuimarisha uwekezaji kwa kutenga bajeti katika michezo ili kukuza na kuibua vipaji vya wanafunzi nchini.

Hayo yamezungumzwa jana Desemba 17, 2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Fatihiya Massawe, ambaye amezindua rasmi Michezo ya 12 ya Umoja wa Michezo ya Vyuo Vikuu Tanzania (Tusa).

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo, Fatihiya amesema michezo hiyo ni jukwaa muhimu linalowaunganisha wasomi wa vyuo vikuu nchini sambamba na kujenga mshikamano wa kitaifa.

Amesema mashindano ya Tusa, yanayofanyika kila baada ya miaka miwili, yamekuwa na mchango mkubwa katika kuunganisha wanafunzi kitaifa na kimataifa, huku yakitoa fursa ya kubaini na kukuza vipaji mbalimbali vya michezo.

“Tunatarajia baada ya mashindano haya kuibuka vipaji vipya vitakavyoendelezwa na hatimaye kulitumikia taifa katika ngazi mbalimbali,” amesema.

Hata hivyo, ameeleza kuwa licha ya vyuo wanachama wa Tusa kufikia 48, ni vyuo 18 pekee vilivyoshiriki mashindano ya mwaka huu, hali aliyosema inahitaji kufanyiwa kazi.

Katika hatua nyingine, aliwakumbusha walimu na wakufunzi wa vyuo vikuu kuendelea kuvitambua, kuviendeleza na kuvikuza vipaji vya wanafunzi kupitia michezo, sambamba na taaluma.

Aidha, aliwataka wakuu wa vyuo vikuu kuhakikisha wanatenga bajeti mahsusi kwa ajili ya michezo ili kuwezesha ushiriki endelevu wa vyuo hivyo katika mashindano ya Tusa bila kukosa.

Kwa upande wao, wadau wa michezo wamehimizwa kushirikiana kwa karibu na Shirikisho la Michezo ya Vyuo Vikuu Tanzania (Tusa) katika kukuza na kuendeleza vipaji vya wanafunzi, ili kuongeza ushindani na tija ya michezo ya vyuo vikuu nchini.