UBORESHAJI VIWANJA VYA NDEGE WAIVUTIA AURIC AIR, YAZINDUA SAFARI MPYA DAR – KAHAMA NA KAHAMA- MWANZA


Uboreshaji wa viwanja vya ndege unaoendelea kufanywa na
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan
umeivutia Kampuni ya Usafiri wa Anga ya Auric Air, ambayo imeanzisha rasmi
safari mpya kati ya Kahama na Dar es Salaam, pamoja na Kahama na Mwanza.

Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo wa
kurahisisha usafiri wa anga na kufungua fursa mpya za biashara na utalii.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa safari hizo, Mkurugenzi wa
Mauzo wa Auric Air, Deepesh Gupta, amesema safari hizo zilianza rasmi Desemba
12, mwaka huu, na kwamba ni hatua muhimu kwa kampuni katika kuboresha
upatikanaji wa usafiri wa anga ulio wa haraka, salama na wa kuaminika nchini.

Gupta amesema safari hizo mpya zimebuniwa mahsusi kukidhi
ongezeko la mahitaji ya usafiri wa anga wenye ufanisi katika ukanda wa Ziwa na
maeneo ya kati nchini.

“Kuimarishwa kwa miundombinu ya usafiri wa anga, hususan katika
Uwanja wa Ndege wa Kahama, kumetuwezesha kuongeza safari hizi. Tunaamini hatua
hii itaongeza ufanisi wa shughuli za kibiashara na kurahisisha ufanyaji wa
biashara kwa wawekezaji na wafanyabiashara kwa ujumla,” amesema Gupta.

Ameeleza kuwa safari hiyo itaendeshwa kwa kutumia ndege ya
Auric Air aina ya Dash 8-300, yenye uwezo wa kubeba abiria 50, inayotambulika
kwa uimara wake, ufanisi wa kiutendaji, mpangilio mpana wa ndani na rekodi
nzuri ya usalama.

Gupta amesisitiza kuwa Kahama ni kitovu muhimu cha uchumi,
hususan katika sekta ya madini na biashara, hivyo kupitia safari hiyo mpya,
Auric Air inalenga kuunga mkono moja kwa moja shughuli za kiuchumi na kuboresha
upatikanaji wa masoko.

Aidha, amesema mbali na safari hizo mpya, Auric Air
inaendelea kuendesha safari nyingine muhimu za ndani ya nchi ikiwemo Dar es
Salaam–Iringa, Dar es Salaam–Arusha na Dar es Salaam–Zanzibar, ambazo amesema
ni nguzo muhimu kwa sekta za biashara, serikali na utalii. 

Kwa upande wake, Ofisa wa Teknolojia, Usimamizi wa
Kumbukumbu na Mipango wa Auric Air, Asha Mzuri, amesema uzinduzi wa safari hizo
mpya utawawezesha wasafiri kusafiri kwa haraka, usalama na urahisi zaidi, hali
itakayochochea shughuli za kiuchumi na kukuza utalii.

“Auric Air tumejikita katika kuunganisha maeneo mbalimbali
ya Tanzania na kuchangia maendeleo ya kitaifa kupitia usafiri wa anga. Uzinduzi
huu ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kupanua mtandao wa huduma zetu ili
kukidhi mahitaji ya wasafiri wote. Tunaendelea kuishukuru Serikali chini ya
uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya anga
nchini,” amesema Mzuri.