Ukosefu wa vyoo watesa makanisa, ofisi za vijiji Maswa

Maswa. Baadhi ya makanisa pamoja na ofisi za watendaji wa vijiji katika Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu, zinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vyoo, hali inayohatarisha afya za wananchi na usalama wa mazingira ya jamii.

Tatizo hili limezua hofu ya kuibuka kwa milipuko ya magonjwa, ikiwemo kipindupindu, hasa wakati huu taifa likielekea katika msimu wa mvua za masika, kipindi ambacho hatari ya kuenea kwa magonjwa ya mlipuko ni kubwa zaidi.

Akizungumza leo, Desemba 18, 2025, katika Kijiji cha Mwasayi, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Anny, amesema kuwa hivi karibuni alipotembelea baadhi ya vijiji, amekuta hali hiyo katika maeneo kadhaa, ikiwemo Kijiji cha Bugarama.

“Nimekuta makanisa matano pamoja na ofisi ya mtendaji wa kijiji hakuna vyoo. Watu wasio na vyoo ni hatari kubwa kwa afya zetu. Mwaka jana Mkoa wa Simiyu ulikumbwa na kipindupindu na chanzo kikubwa ni ukosefu wa vyoo,” amesema.

Dk Anny amewataka wenyeviti wa vitongoji, watendaji wa vijiji, na watendaji wa kata kuhakikisha kuwa kila mwananchi na kila taasisi katika maeneo yao ina choo kinachotumika ipasavyo, ili kuboresha usafi wa mazingira na kuzuia milipuko ya magonjwa.

 “Sheria ipo. Mtu asiye na choo anaweza kufikishwa mahakamani na faini inaanzia Sh50,000 hadi Sh5 milioni. Hatutaki kurudi kwenye kipindupindu. Mimi kama Mkuu wa Wilaya siwezi kukubali hali hii iendelee,” amesema.

Hata hivyo, Mwananchi Digital imebaini kuwa katika baadhi ya vijiji wananchi wanaofika kupata huduma za Serikali au kushiriki ibada za kidini hulazimika kujisitiri vichakani au katika maeneo ya wazi kutokana na kukosekana kwa vyoo, jambo linalochangia uchafuzi wa mazingira na vyanzo vya maji.

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Masela wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano hayupo pichani. Picha na Samwel Mwanga

Akizungumza na Mwananchi Digital, mkazi wa Kijiji cha Bugarama, Daudi Seni amesema tatizo hilo limekuwepo kwa muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

“Ofisi ya kijiji haina choo kabisa. Wananchi wanaokuja kwenye mikutano au kufuata huduma hulazimika kwenda porini. Mvua zikianza, uchafu huu unaingia kwenye maji tunayoyatumia,” amesema. 

Kwa upande Sara Paul mkazi wa kijiji cha Buyubi amesema kuwa kwa taasisi za kidini idadi kubwa ya waumini, hususan siku za ibada na mikutano mikubwa ya kiroho, huongeza uzito wa tatizo hilo.

“Tunapokuwa kwenye  ibada kubwa hasa katika kuelekea sikukuu ya Krismasi changamoto ya vyoo inakuwa kubwa zaidi. Hali hii si salama kiafya wala haiendani na heshima ya maeneo ya ibada,” amesema.

Naye Teleza John ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Matalambuli amesema kuwa ukosefu wa vyoo katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu ni kichocheo kikubwa cha magonjwa ya mlipuko.

“Kipindupindu huenea kwa kasi wakati wa masika endapo mazingira hayazingatii usafi. Ukosefu wa vyoo kwenye ofisi na maeneo ya ibada unaongeza hatari ya kinyesi kuchafua maji na chakula,” amesema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Funika, Jilala Lufunga amesema kuwa changamoto hiyo inasababishwa na ukosefu wa bajeti pamoja na miundombinu duni ya muda mrefu.

“Tunaomba Serikali na wadau wa maendeleo kusaidia ujenzi wa miundombinu hii muhimu, kwani uwezo wetu wa ndani ni mdogo, hasa katika serikali za vijiji,” amesema.