WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema uwekezaji unaoendelea katika sekta ya viwanda na biashara nchini unatarajiwa kufungua fursa kubwa za ajira kwa Watanzania, hususan vijana, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira rafiki ya biashara, kukuza uzalishaji na kupanua masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Desemba 2025, Waziri Kapinga alisema sekta ya viwanda na Judith amesema ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayolenga kujenga uchumi imara, shirikishi na wa kipato cha kati cha juu, kwa kuimarisha viwanda, biashara yenye ushindani na sekta binafsi yenye nguvu.
Ameeleza kuwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita (2021–2024), Serikali imefanya maboresho makubwa ya sera, sheria na kanuni ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuvutia uwekezaji. Maboresho hayo yameongeza kwa kasi usajili wa biashara, leseni na hataza, huku idadi ya viwanda ikiendelea kuongezeka katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Mkoa wa Pwani pekee ambapo viwanda zaidi ya 240 vimeanzishwa ndani ya miaka minne.
“Mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 7.0 mwaka 2023 hadi asilimia 7.3 mwaka 2024, huku sekta ya biashara ikipanda kutoka asilimia 8.4 hadi asilimia 8.6. Ukuaji huo umetokana na uzalishaji mkubwa wa viwandani, uboreshaji wa mazingira ya biashara na kufunguliwa kwa masoko mapya ya kikanda na kimataifa. Amesema Waziri Judith
Amesema Serikali inaendelea kutumia kikamilifu fursa za masoko ya kikanda na kimataifa ikiwemo Soko Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), Umoja wa Ulaya na Asia, ambapo mauzo ya nje ya bidhaa za Tanzania yameendelea kuongezeka, yakichangiwa na mazao ya kilimo yaliyoongezwa thamani, bidhaa za viwandani na madini.
Hali hiyo, amesema, inatoa nafasi kubwa kwa vijana kuanzisha biashara za uzalishaji na mauzo ya nje.
Waziri Judith amebainisha kuwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama Mchuchuma na Liganga, Magadi Soda Engaruka, Maganga Matitu na Katewaka, unatarajiwa kutoa maelfu ya ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, hasa kwa vijana wenye ujuzi wa ufundi, uhandisi, uchimbaji, usambazaji na biashara.
Vilevile, Serikali inaendelea kuwekeza katika kongani za viwanda, ambapo hadi sasa zipo kongani 34 nchini. Miongoni mwao ni Kwala Industrial Park na Modern Industrial Park Mlandizi, zinazotarajiwa kuajiri makumi ya maelfu ya vijana na kuwa vituo vya ubunifu, teknolojia na biashara.
Katika hatua nyingine, Waziri Judith amesema Serikali inaweka mkazo kwenye maendeleo ya viwanda vidogo, ubunifu na biashara mtandao kama maeneo mapya ya ajira kwa vijana. Kupitia taasisi kama SIDO, TIRDO, TEMDO na CAMARTEC, vijana wanapatiwa mafunzo, teknolojia, mitaji na masoko ili kukuza biashara zao na kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kuhusu mitaji, Waziri Judith amesema Serikali kupitia mifuko na taasisi za fedha imeendelea kutoa mikopo ya riba nafuu kwa wajasiriamali, ambapo maelfu ya vijana wamenufaika na mikopo hiyo kwa ajili ya kuanzisha na kukuza viwanda vidogo, biashara za uzalishaji na ubunifu wa teknolojia.
Akihitimisha, Waziri Judith amewahimiza vijana kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya viwanda na biashara, akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka msingi imara wa Tanzania ya viwanda, na iko tayari kuwa mshirika wa karibu wa vijana katika safari ya kujenga uchumi wa kisasa, shindani na jumuishi.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa kweny mkutano na waziri wa Biashara na Viwanda, Judith Kapinga.
