WAHIFADHI TFS SAO HILL WAJENGEWA UELEWA WA AFYA

Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Tebby Yoramu,akiwa anapima afya akiwaongoza watumishi wengine wa Zao Hill kupima afya zao na amesema mafunzo hayo hutolewa kila mwaka kama sehemu ya mafunzo endelevu kwa watumishi wa TFS, yakilenga kuwajengea uwezo wa kujikinga na magonjwa yanayoathiri afya na kushusha kasi ya utendaji kazi.

Wahifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutoka Shamba la Miti Sao Hill wamepatiwa mafunzo maalumu kuhusu masuala ya afya, yakilenga kuongeza uelewa juu ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) pamoja na magonjwa yasiyoambukiza, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha ustawi wao na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi wa misitu.

Na Fredy Mgunda, Mufindi Iringa

Mafunzo hayo yamelenga kuwaelimisha wahifadhi kuhusu hali halisi ya maambukizi ya VVU, njia za kujikinga, umuhimu wa upimaji wa hiari na wa siri, pamoja na kuondoa dhana potofu zinazokwamisha juhudi za kudhibiti maambukizi. Washiriki walikumbushwa kuzingatia maadili, kujilinda na kuchukua tahadhari stahiki katika maisha ya kila siku.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Sao Hill, PCO Tebby Yoramu, amesema mafunzo hayo hutolewa kila mwaka kama sehemu ya mafunzo endelevu kwa watumishi wa TFS, yakilenga kuwajengea uwezo wa kujikinga na magonjwa yanayoathiri afya na kushusha kasi ya utendaji kazi.

“Afya njema ni mtaji muhimu katika kulinda rasilimali za misitu, kwani kazi ya uhifadhi inahitaji nguvu, umakini na utayari wa mwili na akili. Ni muhimu kuzingatia maelekezo ya wataalamu ili kujikinga na magonjwa mbalimbali,” amesema PCO Yoramu.

Katika mafunzo hayo, mada za magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya moyo na saratani zilijadiliwa kwa kina. Wahifadhi walielimishwa kuhusu dalili za awali, visababishi na athari za magonjwa hayo kwa afya na ufanisi wa kazi.

Washiriki walihimizwa kubadili mtindo wa maisha kwa kuzingatia lishe bora, kufanya mazoezi ya mara kwa mara, kudhibiti msongo wa mawazo na kuepuka matumizi ya pombe kupita kiasi pamoja na uvutaji wa sigara, ambavyo vimetajwa kuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya magonjwa yasiyoambukiza.

Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Dkt. Bonaventura Chitopela, amesema kila mmoja ana wajibu wa kulinda afya yake kwa kupima afya mapema na kufuata ushauri wa wataalamu ili kupata matibabu kwa wakati.

“Tumia fursa hizi kupima afya zenu mara kwa mara ili kujua hali za kiafya mapema, hatua itakayowezesha kupata matibabu na ushauri kwa wakati,” amesema Dkt. Chitopela.

Kwa upande wake, Mkufunzi kutoka TACAIDS na Meneja wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bw. Emmanuel Petro, amewataka wahifadhi kutumia kikamilifu elimu waliyoipata kwa kuchukua hatua za mapema dhidi ya changamoto za kiafya, akisisitiza kuwa uzingatiaji wa maelekezo ya wataalamu ni msingi wa kuzuia madhara ya kiafya.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za TFS kuhakikisha wahifadhi na watumishi wake wanakuwa na afya bora, nidhamu na uwajibikaji. Wahifadhi walioshiriki wameahidi kuzingatia elimu waliyoipata na kuwa mabalozi wa afya njema katika maeneo yao ya kazi na jamii zinazowazunguka.