Kigoma. Wahitimu na wanafunzi wa vyuo mbalimbali nchini wanaosoma fani ya uandishi wa habari, wameshauriwa kuongeza ujuzi wao katika masuala ya kidijitali, ikiwemo matumizi sahihi ya akili mnemba (AI), ili kuepusha matumizi mabaya ya teknolojia yanayoweza kupotosha umma.
Rai hiyo imetolewa leo Alhamisi, Desemba 18, 2025 na Mkuu wa Maudhui ya Mtandaoni wa Azam Media, Hassan Mhelela wakati wa mahafali ya kwanza ya Chuo cha Habari na Utangazaji cha Ujiji (UBA) kilichopo mjini Kigoma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhelela amesema mabadiliko ya teknolojia duniani yameifanya tasnia ya habari kuhitaji waandishi wenye ujuzi mpana wa masuala ya mtandaoni, ikiwemo matumizi sahihi ya vifaa vya kidijitali, sambamba na kuzingatia sheria na taratibu za kitaaluma.
“Dunia inaendelea kubadilika kwa kasi, na sasa kuna matumizi ya akili mnemba. Hata hivyo, ni muhimu kwa waandishi wa habari kufahamu matumizi sahihi ya teknolojia za kidijitali ili kuendana na mabadiliko ya ulimwengu wa sasa,” amesema Mhelela.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha UBA, Victoria Ndekeye amesema mahafali hayo ni mwanzo wa safari ya kitaaluma kwa wahitimu hao, akiwataka kwenda kuyatekeleza kwa vitendo yale waliyofundishwa chuoni, huku wakitanguliza maslahi ya wananchi.
“Wekeni mbele maslahi ya wananchi popote mtakapofanya kazi, msiegemee upande wowote na muendelee kufanya kazi kwa kujituma, haki na nidhamu ya hali ya juu,” amesema Ndekeye.
Akizungumza kwa niaba ya wazazi, Abel Laurent amesema kuhitimu kwa wanafunzi hao si mwisho wa kujiongezea maarifa, akieleza kuwa uandishi wa habari ni fani inayohitaji kujifunza na kufuatilia kwa karibu yanayoendelea duniani.
Naye Aisha Masoud amesema katika mazingira ya sasa ya mitandao ya kijamii ambapo karibu kila mtu anaweza kuchapisha taarifa, wahitimu wa uandishi wa habari wanapaswa kujitofautisha kwa kufanya kazi kwa weledi, kuzingatia taaluma na maadili waliyofundishwa.
