Wamiliki vituo vya mafuta Mbeya watakiwa  kukagua pampu kabla ya kutoa huduma

Mbeya. Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Mbeya imesema haitosita kuchukulia hatua wamiliki wa vituo vya mafuta watakaobainika kushindwa kukagua pampu kabla ya kutoa huduma kwa mlaji wa mwisho.

WMA imesema kuwa hatua hiyo inalenga kudhibiti uchezeshwaji wa mifumo ya usambazaji wa mafuta wakati wa mauzo, jambo ambalo mara nyingi husababisha wateja kulipia huduma isiyoendana na thamani halisi ya fedha waliyonunua.

Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Mbeya, Hassan Mrisho, ameliambia Mwananchi Digital leo Desemba 18, 2025, kuhusu mikakati ya kufanya uhakiki na ukaguzi wa kushtukiza kwenye vituo vya mafuta ili kubaini uhalisia wa utoaji huduma kupitia mifumo ya pampu za mafuta.

Amesema kuwa, licha ya kaguzi za mara kwa mara, WMA bado inaendelea kutoa elimu kwa wamiliki wa vituo vya mafuta, wakikumbushwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Vipimo, Sura Namba 340, mapitio ya mwaka 2023, ambayo inalenga kumlinda mlaji ili apate bidhaa kulingana na thamani halisi ya fedha.

“Tunatoa elimu kwa wamiliki wa vituo vya mafuta kujua umuhimu wa kufanya ukaguzi wa pampu kabla ya kuanza kutoa huduma na endapo zina changamoto watoe taarifa ili kukwepa mkono wa sheria,” amesema.

Mrisho amesema ili kuhakikisha wanalinda walaji wa mwisho wa bidhaa za mafuta wameweka mikakati ya kufanya operesheni za kushtukiza ili kuwabaini wanaokiuka kwa makusudi au uzembe kwa masilahi yao binafsi.

Kwa upande wake, dereva wa bodaboda katika Kijiwe cha Mabatini, Jiji la Mbeya, Erasto Mwakalonge, amesema kuwa mfumo wa ukaguzi wa mara kwa mara utawasaidia wateja kupata bidhaa kulingana na thamani halisi ya fedha wakati wa kununua mafuta.

“Unajua kuna wakati unaweza kununua mafuta ya Sh5,000, lakini ukasafirisha abiria kwa saa kadhaa yanakata jambo ambalo limekuwa mwiba mkali kwetu,” amesema.

Mwakalonge amesema  wanaomba mamlaka husuka  kuweka mkazo wa ukaguzi wa kushtukiza ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Kwa upande wake, msimamizi wa Kituo cha Mafuta cha Puma, Khalid Yahaya, amesema kuwa ni wakati kwa wafanyabiashara wa vituo vya mafuta kutekeleza maelekezo ya Serikali ili kuhakikisha wateja wanapata huduma bora na bidhaa kulingana na thamani halisi ya fedha.

“Utaratibu wa  pampu ya kusukuma mafuta uko kwenye mfumo maalumu, lakini ni wajibu wetu kabla ya mauzo  kuzikagua kujiridhisha  ili kukwepa mkono wa sheria,” amesema.