Unguja. Meneja wa Kitengo cha Uhusiano wa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF), Asha Kassim Biwi amesema kuwa bado kuna changamoto kwa baadhi ya wananchi kutoelewa kikamilifu huduma zinazotolewa na mfuko huo, hali inayosababisha upotoshaji na matumizi duni ya fursa zilizopo.
Biwi ameyasema hayo leo Alhamisi, Desemba 18, 2025 wakati akitoa mada katika mkutano wa wanahabari na washawishi uliofanyika Rahaleo, Mjini Unguja.
Amesema uanzishwaji wa mfuko huo ni miongoni mwa mipango ya Serikali yenye lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya, bila kukabiliwa na vikwazo vya kifedha. Amesema wananchi wanahimizwa kujiunga na mfuko huo ili kukusanya rasilimali fedha zitakazogharamia huduma za matibabu.
“Mfuko huu umeanzishwa kwa lengo la kuwanunulia wananchi huduma za afya ikiwemo dawa, vipimo na huduma nyingine, ambazo upatikanaji wake umekuwa changamoto kutokana na ongezeko la wananchi,” amesema Asha.
Ameongeza kuwa utaratibu wa matumizi ya mfuko huo bado ni mgeni kwa baadhi ya wananchi, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ili kuondoa upotoshaji uliopo kuhusu huduma zinazotolewa.
Amefafanua kuwa wanachama wa ZHSF wananufaika kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na wasiokuwa wanachama, ambao mara nyingi hulazimika kugharamia matibabu kwa gharama kubwa, hali inayowafanya wengine kuuza mali zao ili kupata huduma za afya.
Kwa upande wake, Ofisa Msimamizi wa Usajili wa Wanachama wa ZHSF, Bakari Ali Bakari amesema hadi sasa jumla ya wanachama 978,000 wamesajiliwa rasmi tangu kuanzishwa kwa mfuko huo na wanaendelea kunufaika na huduma zake.
Bakari amefafanua kuwa ada ya mwaka inalipwa kulingana na makundi ya kijamii, watu wa tabaka la juu hulipa Sh560,000, wa hali za kati Sh420,000 na wa hali ya chini Sh490,000. Amesema kwa wananchi wa hali ya chini, sehemu ya gharama hizo huchangiwa na Serikali, hivyo fedha hizo hazitoki mifukoni mwao kama ilivyo kwa makundi mengine.
Aidha, Bakari amesema wageni wanaoishi Zanzibar kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita, hulipa asilimia saba ya mshahara wao kwa mwezi, huku mgeni anayekuja Zanzibar kwa ajili ya shughuli za uchumi au utalii akitakiwa kulipia dola 500 za Marekani.
Bakari ametoa wito kwa wananchi kujiunga na mfuko huo ili kuondokana na changamoto za upatikanaji wa huduma bora za afya na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Naye mshiriki wa mkutano huo, Juma Haji Juma amesema awali hakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mfuko huo, lakini baada ya kupata elimu katika mkutano huo ameahidi kuwa mstari wa mbele kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi kuhusu ZHSF na manufaa yake.