Wananchi Dar walia bili kubwa za maji bila maji

Dar es Salaam. Katikati ya kilio cha ukosefu wa huduma ya maji safi na salama katika baadhi ya maeneo jijini Dar es Salaam, kumeibuka changamoto nyingine kwa wananchi kulalamikia kutumiwa ankara kubwa za huduma hiyo, hali inayowaathiri zaidi wa kipato cha chini.

Hata hivyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), Mkama Bwire alipoulizwa kuhusu ankara kubwa na gazeti hili leo Desemba 18, 2025, amesema changamoto hiyo inamhusu mteja mmoja mmoja na amewataka wananchi kufika katika mamlaka hiyo ili ifanyiwe kazi.

Akizungumza kuhusu malalamiko ya ankara za maji, Bwire amesema kupata huduma ya maji kwa mgawo haimaanishi mteja hapati huduma.

Amefafanua kuwa wateja wote wa Dawasa wanatumia mita zinazopima kiasi halisi cha maji kinachotumika, ingawa wakati mwingine mita hizo zinaweza kuwa na changamoto za kiufundi.

“Endapo mteja anaona bili haieleweki, anapaswa kupiga simu namba 181 bure au kufika Dawasa ili kusaidiwa. Hata kama kuna mgawo wa maji, hiyo haimaanishi hakuna huduma,” amesema Bwire.

Baadhi ya watumiaji wa maji wamesema ankara kubwa za maji wanazopata hazilingani na kiwango halisi cha matumizi yao, hali inayoongeza mzigo wa gharama.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wakazi hao wamesema licha ya kutumia maji kwa kiwango kidogo, wamekuwa wakipokea ankara kubwa zisizoelezeka, jambo linalowatia wasiwasi kuhusu uhalali wa bili wanazotozwa.

Mkazi wa Tabata Sanene, Baltazar Amos amesema changamoto hiyo ni ya muda mrefu na si ya kipindi cha sasa, huku juhudi zake za kuwasiliana na mamlaka zikigonga mwamba.

“Changamoto hii ni ya muda mrefu. Kila nikipiga simu hawapokei kusikiliza kilio changu. Mara nyingi simu inaita bila kupokewa, jambo linalonifanya nijiulize kinachoendelea. Hata nikijaribu kuwasilisha malalamiko kupitia mitandao yao ya kijamii, hawajibu,” amesema Amos.

Kwa upande wake, Mariam Sambrina, mkazi wa Mabibo, amesema licha ya kupata maji kwa mgawo, bili anazotumiwa hazilingani na uhalisia wa matumizi yake.

“Miezi mitatu iliyopita nilikuwa nalipa Sh16,000 kwa mwezi wakati huo nilikuwa na watoto wangu. Hata baada ya watoto kwenda shule, bili imeendelea kuwa kiwango kilekile, ilhali muda mwingi niko kazini,” amesema Mariam.

Ameongeza kuwa hali hiyo inamuumiza zaidi kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, akisema kuongezewa gharama zisizo na uhalisia kunazidi kumwekea shinikizo la maisha.

“Ni muhimu mamlaka kulichukulia suala hili kwa uzito. Kama mita zina hitilafu, zibadilishwe badala ya kuwatumia wananchi bili kubwa. Wasiwasi wangu ni kwamba huenda wasomaji wa mita hawafanyi uhakiki wa kina, bali wanakadiria matumizi,” amesema.

Naye Richard Richard, mkazi wa Tabata Kisiwani, amesema bili kubwa za maji zimekuwa changamoto sugu katika nyumba wanayoishi, akibainisha hata baada ya kufuatilia suala hilo kwa mamlaka husika hakupata majibu ya kuridhisha.

“Tunaishi wapangaji kadhaa, wengi wetu ni wasela na tunakuwa nyumbani zaidi Jumamosi na Jumapili. Hatutumii maji kwa kiwango kikubwa kwa kuwa hatuna vyombo vingi, lakini bado bili ni kubwa,” amesema Richard.

Katika hatua nyingine, Bwire ameongeza kuwa hata katika vipindi ambacho hakuna changamoto ya upatikanaji wa maji, bado mamlaka imekuwa ikipokea malalamiko kama hayo.

Amesema kabla ya bili kutumwa, Dawasa hutuma ujumbe kwa mteja ili kuthibitisha usomaji wa mita na kuhakikisha kiasi kilichosomwa ndicho kinachoonekana.

“Baada ya uhakiki huo ndipo bili hutumwa. Ni muhimu kuelewa kuwa inawezekana mteja kukosa maji kwa siku tatu au nne, lakini siku maji yanapopatikana hujaza kwenye vyombo na kuyatumia kwa siku nyingine,” amesema Bwire.