Arusha. Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amewataka wataalamu wanaotekeleza miradi ya usafirishaji nchini kuhakikisha inachangia ukuaji wa uchumi wa Taifa, huku ikilinda mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadaye.
Kauli hiyo imetolewa leo wakati wa kufunga mkutano wa 18 wa Tathmini ya Pamoja ya Sekta ya Usafirishaji (JTSR), ambapo Waziri Mbarawa aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkude amesema kuwa sekta ya usafirishaji ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi, hivyo inapaswa kuendeshwa kwa kuzingatia misingi ya maendeleo endelevu, ulinzi wa mazingira, na ustawi wa jamii.
“Sekta ya usafirishaji lazima iunganishe masuala ya ulinzi wa mazingira, kupunguza na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuzingatia hatua za ulinzi wa kijamii katika upangaji, ujenzi, na uendeshaji wa miundombinu na huduma zake,” amesema.
Akirejelea Mpango wa Hatua wa Sekta ya Usafirishaji Kuhusu Mazingira (TSEAP 2025–2030), Mkude amesema Serikali inalenga kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa, kuhamasisha na kukuza matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira, kuimarisha uzingatiaji wa masuala ya mazingira, na kuongeza uwezo wa taasisi katika sekta ya usafirishaji.
Amesisitiza kuwa utekelezaji wa mpango huo unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, taasisi zake, washirika wa maendeleo, sekta binafsi na jamii kwa ujumla.
“Ni muhimu wadau wote kuumiliki mpango huu na kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha sekta ya usafirishaji inaendelea kuchochea ukuaji wa uchumi bila kuathiri mazingira, kwa masilahi ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema.
Mkutano huo, umefanyika jijini Arusha, ukiwa na kauli mbiu “Mfumo Jumuishi wa Usafirishaji Kama Msingi wa Mageuzi ya Kiuchumi kuelekea Dira ya Maendeleo 2050”, umelenga kutathmini utekelezaji wa sera, mipango, na miradi mbalimbali ya sekta ya usafirishaji nchini.
Ambapo umewakutanisha wadau wakuu wa sekta ya usafirishaji wakiwemo wawakilishi wa Serikali, washirika wa maendeleo, taasisi za umma na binafsi, pamoja na asasi za kiraia.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara amesema mkutano huu hufanyika kila mwaka kama jukwaa la kuwakutanisha wataalamu wa sekta ya usafirishaji, hususan wa ujenzi wa barabara, reli, na bandari, ili kupanga kwa pamoja na kutatua changamoto za utekelezaji wa miradi.
Profesa Kahyarara ameongeza kuwa sekta ya usafirishaji kwa sasa inachangia zaidi ya asilimia 10 ya ajira nchini, ikiwahusisha watu wapatao milioni tatu, na kuingiza mapato ya zaidi ya dola bilioni 2.66, huku faida zake zikitarajiwa kuongezeka zaidi katika miaka ijayo.