Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu amewaagiza viongozi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), kuendelea kuchukua hatua kali zaidi za kisheria dhidi ya waajiri wa sekta binafsi wanaoshindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati.
Amesisitiza kwamba kitendo hicho kinawanyima wafanyakazi haki zao za msingi, ikiwamo ya mafao ya uzeeni.
Sangu ametoa maelekezo hayo leo Alhamisi Desemba 18, 2025 wakati wa ziara yake ya kikazi katika Ofisi za NSSF jijini Dodoma, ikiwa ni ya kwanza tangu alipoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo.
Katika ziara hiyo, ameambatana na Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Mahusiano, Rahma Kisuo.
Amesema ni wajibu wa kisheria kwa kila mwajiri wa sekta binafsi kujiandikisha katika mfuko, kuwaandikisha wafanyakazi wake na kuwasilisha michango yao kwa wakati kila mwezi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi katika Ofisi za NSSF jijini Dodoma.
Waziri huyo amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia uzembe au makusudi ya kukiuka sheria kwa waajiri wanaohatarisha mustakabali wa wafanyakazi wao.
“Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, hakikisha waajiri wote wasiowasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati wanachukuliwa hatua za kisheria bila muhali, kwani wanaposababisha kucheleweshwa kwa mafao, huwaumiza wafanyakazi waliolitumikia Taifa kwa muda mrefu,” amesema Waziri Sangu.
Aidha, ameipongeza NSSF kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita, akitaja ongezeko la wanachama na waajiri.
Amesema pia NSSF imeendelea kuimarika katika makusanyo ya michango, mapato ya uwekezaji, kuongezeka kwa thamani ya mfuko pamoja na maboresho ya malipo ya mafao kwa wanachama.
Awali akitoa taarifa ya utendaji wa Mfuko, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema katika kipindi cha miaka mitano kilichoishia Juni 30, 2025, mfuko umeongeza idadi ya wanachama wapya kutoka 215,693 mwaka 2020/21 hadi 363,925 mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 68.72.
Amesema katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26, mfuko uliandikisha wanachama wapya 111,881, sawa na asilimia 110 ya lengo, huku kwa mwaka mzima wa fedha 2025/26 unatarajiwa kuandikisha wanachama wapya 447,523, wakiwemo 316,957 kutoka sekta rasmi na 130,566 kutoka kwa wananchi waliojiajiri.
Mshomba amesema hadi kufikia Septemba 30, 2025, idadi ya wanachama wachangiaji imeongezeka na kufikia 1,703,821 ikilinganishwa na 932,112 waliokuwepo Juni 2021, sawa na ongezeko la asilimia 82.79, huku makusanyo ya michango yakiongezeka kutoka Sh1,171.97 bilioni hadi kufikia Sh2,718.87 bilioni huku thamani ya mfuko ikifikia Sh10 trilioni.