Bajaji za umeme zinavyogusa maisha na kulinda mazingira

Dar es Salaam. Siku moja akiwa Ubungo, jijini hapa akisubiri abiria kama ilivyokuwa desturi yake, Makoni Francisco (47), alifanya uamuzi uliobadilisha kabisa maisha yake.

Aliamua kuacha pikipiki yake ya matairi matatu maarufu kama bajaji iliyokuwa inatumia petroli na kuanza kutumia ya umeme.

Miaka miwili imepita tangu alipofanya uamuzi huo, maisha yake yamebadilika. Akiegesha bajaji yake katika kituo cha njiapanda ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Francisco sasa huingiza kati ya Sh40,000 na Sh50,000 kwa siku, huku akitumia kiasi kidogo kulipia umeme wa kuchaji betri. Akilinganisha na kipindi cha nyuma, anasema” “nilipata Sh40,000 kwa nadra sana”.

Kupungua kwa gharama zitokanazo na ununuzi wa mafuta, kumemwezesha kuongeza faida na kuimarisha kipato chake cha kila siku.

“Bajaji hii haina kelele, wateja wangu wanaipenda na sasa nimesahau kabisa habari ya petroli. Kwa bajaji hii nasomesha watoto wangu na nina sehemu ya kuishi. Inanipa kipato cha kuendesha maisha.”

Francisco hayuko peke yake, Tanzania inashuhudia ongezeko la bajaji na pikipiki za umeme hasa katika majiji makubwa kama Dar es Salaam na Dodoma.

Anaunga mkono haya, Majidi Rashidi dereva bajaji kati ya Manzese na Mbezi ambaye alianza matumizi ya chombo hicho miezi minane iliyopita.

Serikali kuweka msukumo kupitia sera za nishati safi na motisha kwa wawekezaji, kuwawezesha wajasiriamali wadogo kama Francisco kuingia kwenye mfumo huu mpya wa usafiri nafuu.

Zaidi ya kuboresha kipato cha madereva, bajaji za umeme zinasaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kupungua kwa moshi na kelele kunaleta unafuu kwa wakazi wa Dar es Salaam na miji mingine yenye msongamano mkubwa wa watu.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa (UN), nishati za kisukuku ikiwemo makaa ya mawe, mafuta na gesi zinachangia zaidi ya asilimia 75 ya uzalishaji wa hewa joto duniani na karibu asilimia 90 ya uzalishaji wote wa hewa ya kaboni dioksidi. Nishati hizo hutumiwa zaidi na vyombo vya moto, zikiwemo bajaji.

Tofauti na bajaji zinazotumia injini za mafuta, ambazo hutoa takriban tani tatu za gesi chafuzi kila mwaka kwa mujibu wa UN, bajaji za umeme zinaweza kutokuwa na uzalishaji kabisa wa gesi hizo endapo zitatumia nishati mbadala ikiwemo umeme.

Afisa Mawasiliano na Uchechemuzi kutoka Amshaamsha Foundation, Zakia Mrisho anasema matumizi ya umeme kuendesha vyombo vya moto ikiwemo bajaji yanasaidia kupunguza uzalishaji wa hewajoto ambayo imekuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira.

“Mafuta kama petroli yanazalisha sana hewa chafu ambayo imekuwa zikichangia ongezeko la joto, kina cha bahari na mabadiliko ya unyeshaji wa mvua, lakini tukitumia umeme athari hizo zitapungua zaidi,” anasema Zakia.

Zakia ambaye taasisi yake imejikita katika uchechemuzi wa mabadiliko ya tabianchi, anasema bajaji za umeme zinapunguza uchafuzi wa hewa hasa katika maeneo yenye msongamano mkubwa watu kama Dar es Salaam na gharama za uendeshaji kwa wamiliki.

Fundi wa mfumo wa umeme wa bajaji katika kampuni ya teknolojia ya usafiri wa umeme ya Ekoglobe, Abou Mdumbwa wa Sinza, Dar es Salaam, anasema bajaji za umeme ni bora zaidi kuliko zinazotumia mafuta kwa sababu hazipigi kelele zikiwa barabarani na humpunguzia gharama ya uendeshaji mtumiaji.

“Hizi bajaji ni imara, hata betri lake linaweza kukaa zaidi ya miaka mitano (sawa na kuchaji zaidi ya mara 7,000) bila kubadilishwa,” anasema Mdumbwa.

“Betri la bajaji linaweza kuchajiwa mahali popote penye umeme wa uhakika.”

Mathalani, kwa lita moja ya petroli, bajaji ya kawaida inaweza kusafiri takribani kilomita 20 na kugharimu karibu Sh3,159. Kusafiri umbali huohuo kwa kutumia bajaji ya umeme hugharimu Sh527 tu. Upungufu huu ni karibu mara sita ya gharama.

Pia, akiba hii ya gharama inaweza kufidia tofauti ya bei kati ya bajaji ya umeme na ya kawaida ndani ya kipindi cha miezi sita hadi nane.

Ekoglobe ambayo ilianza shughuli zake Tanzania mwaka 2020 inalenga kuingiza bajaji 5,000 nchini ndani ya kipindi cha miaka mitano. Pia iko katika mpango wa kuifikia mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Arusha, Singida, Shinyanga, Geita na Kilimanjaro.  Kwa sasa, inatoa huduma katika mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Mwanza na Dodoma.

“Muitikio umekuwa mzuri hasa kwa madereva kwa sababu wanaokoa gharama za maisha,” anasema Clinton Elias, ofisa usafiri wa Ekoglobe akibainisha kuwa bajaji za umeme zinauzwa kwa bei nafuu kati ya Sh1.5 milioni na Sh5 milioni.

Pia kulingana na aina zipo zinazouzwa hadi Sh8 milioni. Pesa hizi ni ndogo ikilinganishwa na zaidi ya Sh10 milioni ya bajaji za petroli.

Tangu mwaka 2019, Tanzania imekuwa ikishirikiana na Mpango wa kimataifa wa usafiri wa umeme wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), kupitia mradi wa SolutionsPlus, ambao husaidia kampuni changa zinazochagiza matumizi ya usafiri wa umeme.

Mradi huu unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) unasaidia kusambaza pikipiki na bajaji za umeme kwa kutoa ushauri wa sera na ufadhili kwa kampuni hizo kuwafikia watu wengi ili kuokoa mazingira na kutengeneza ajira.

Hatua hizo za matumizi ya bajaji za umeme nchini Tanzania ni sehemu ya mabadiliko makubwa katika sekta ya usafirishaji Afrika.

Kufikia mwaka 2020, bara hilo lilikuwa na jumla ya pikipiki na bajaji za umeme milioni 27, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya UNEP iitwayo “Pikipiki na Bajaji za Umeme: Muhtasari wa Soko Linalokua Duniani” iliyotolewa Januari mwaka 2024.

Afisa Mikopo wa DEEM Finance, Aggrey Mushi anasema mikopo wanayotoa inalenga kuchochea ukuaji wa sekta hii kwa kuwawezesha madereva, hususani vijana na wanawake, ili waweze kumiliki bajaji na pikipiki za umeme bila kikwazo.

“Vyombo hivi vya umeme vina gharama kuvimiliki na ni changamoto kwa madereva wengi kulipia malipo yote kwa mkupuo mmoja, mikopo yetu hutolewa kwa mfumo wa ‘Lease to Own’, na unawapa uwezo madereva kulipia kidogokidogo huku wakijiajiri wenyewe kwenye ajira hizi za kijani,” anasema Mushi.

Mikopo hiyo inalenga kujenga mfumo wa biashara ya usafirishaji ambao ni rafiki kwa mazingira na wenye faida kiuchumi kwa wadau wote, kuanzia madereva, wateja, hadi kampuni zinazosambaza bajaji hizo.

Mpaka sasa, taasisi hiyo imetoa mikopo ya bajaji na bodaboda kwa madereva 150 kwa kushirikiana na wasambazi wa vyombo hivyo.

“Ni vyema ikafahamika kuwa madereva hawa hawapewi fedha taslimu, isipokuwa wananunuliwa chombo wanachokihitaji na kuruhusiwa kukikodisha mpaka pale wanapokamilisha marejesho yao  ndio umiliki unahama rasmi,” anasisitiza Mushi.