BENKI YA STANBIC YATOA VIFAA TIBA TAASISI YA MOYO MUHIMBILI

Katika kuendelea kuunga mkono sekta ya afya nchini, Benki ya Stanbic Tanzania imetoa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 19.9 kwa Taasisi ya Moyo Hospitali ya Muhimbili, hatua inayolenga kuboresha utoaji wa huduma afya kwa wananchi ili kuongeza ufanisi wa huduma ndani ya hospitali hiyo.

Akikabidhi vifaa tiba hivyo Meneja wa Benki ya Stanbic mkoa wa Dar es salaam Bi. Edditrice Marco kwa Mkurugenzi wa Kitengo cha Moyo hospitali ya Muhimbili, Dkt. Tatizo Waane alisema msaada huo umetolewa kupitia mpango wa uwajibikaji kwa jamii (CSI), ukiendeleza sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 tangu benki ilipoanza kutoa huduma nchini.

Tunatambua umuhimu wa sekta ya afya katika ustawi wa jamii. Kupitia msaada huu tunalenga kuboresha huduma kwa wagongwa na kusaidia watoa huduma kuongeza ufanisi. Hii ni moja ya njia tunazosherehekea miaka 30 ya kukua pamoja na Watanzania. Alisema Bi. Edditrice.

Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha Moyo hospitali ya Muhimbili, Dkt. Tatizo Waane ameishukuru Benki ya Stanbic kwa kuwapatia vifaa hivyo, huku akitoa wito kwa mashirika binafsi kuendelea kujitolea ili kuboresha zaidi sekta ya afya nchini.
Meneja wa benki ya Stanbic mkoa wa Dar es salaam, Edditrice Marco (wapili kushoto) akimkabidhi Mkurugenzi wa Kitengo cha Moyo hospitali ya Muhimbili, Dkt. Tatizo Waane vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 19.9 kutoka benki ya Stanbic ikiwa sehemu ya benki hiyo kurudisha kwa jamii CSI. Wengine kulia ni Mkurugenzi wa Uuguzi, Robert Mallya na kushoto ni Kaimu Meneja wa Tawi la Kariakoo Stanbic, Grace Obadia.