Simanjiro. Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Festo Lulandala amepiga marufuku shughuli za usafishaji wa mashamba mapya kwa ajili ya kilimo Kata ya Langai, hatua inayolenga kutoa fursa ya kuchunguza na kusuluhisha migogoro ya ardhi inayolikumba eneo hilo.
Hata hivyo, Lulandala ameunda kamati ya watu saba itakayokuwa na jukumu la kufanya uchunguzi wa kina kuhusu migogoro ya ardhi inayotarajiwa kukamilisha kazi yake ifikapo Januari 15, 2026.
Mkuu huyo wa wilaya ametoa kauli hiyo leo Ijumaa, Desemba 19, 2025, alipokuwa akizungumza na wakazi wa Kata ya Langai, baada ya kusikiliza kero, malalamiko na changamoto mbalimbali zinazohusiana na umiliki na matumizi ya ardhi katika eneo hilo.
Amesisitiza kuwa kutokana na kutotolewa vibali halali vya kusafisha mashamba mapya, ameagiza kusitishwa mara moja kwa shughuli zote za usafishaji wa mashamba mapya katika kata hiyo, hadi pale migogoro ya ardhi itakapopatiwa ufumbuzi wa kudumu.
“Kwa sababu vibali vipya vya kusafisha mashamba havijatolewa, napiga marufuku usafishaji wa maeneo ya mashamba mapya hadi itakavyoelekezwa upya,” amesema Lulandala.
Ameeleza kuwa, hatua ya kuunda kamati hiyo ya watu saba inalenga kufanya uchunguzi wa kina kuhusu migogoro ya ardhi katika eneo hilo na kutoa mapendekezo yatakayowezesha kupatikana kwa suluhisho la kudumu.
“Miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo ni ofisa ardhi wa wilaya, ofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), mtendaji wa Kata ya Langai, askari polisi na ofisa maendeleo ya jamii wa kata,” amesema Lulandala.
Mmoja wa wakazi wa Kata ya Langai, Sakita Santana, amesema baadhi ya watu wenye ushawishi wamevamia maeneo ya ardhi ya wananchi, hali iliyosababisha kuibuka kwa migogoro.
Ameitaka Serikali kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika.
Santana amesema baadhi ya watu wenye uelewa wa kisheria wanadaiwa kuandaa ramani bandia za ardhi kwa lengo la kujinufaisha binafsi na kuuza maeneo hayo kwa wananchi wasio na taarifa sahihi.
Mkazi mwingine wa kata hiyo, Mokia Sipitieck, amelalamikia ugawaji holela wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya malisho ya mifugo na kilimo, hali inayochochea migogoro ya ardhi katika eneo hilo.
Sipitieck amesema baadhi ya maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya nyanda za malisho yamevamiwa na shughuli za kilimo kinyume na mpango wa matumizi bora ya ardhi, jambo analodai linahatarisha ustawi wa wafugaji na wakulima kwa jumla.