Iringa. Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, amewaagiza viongozi wa vijiji, kata na halmashauri kuhakikisha mapato ya Jumuiya ya MBOMIPA yanawanufaisha wananchi moja kwa moja kwa uwazi, uwajibikaji, na matumizi sahihi ya fedha za utalii.
DC Sitta ameyasema hayo Desemba 19, 2025, wakati wa kikao cha uwasilishwaji wa taarifa ya maendeleo ya MBOMIPA 2024/2025 kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa Chuo Huria, Manispaa ya Iringa.
Amesema mafanikio ya jumuiya yanapaswa kuakisi maendeleo halisi ya kijamii, na siyo kutumika kwa shughuli zisizo na tija.
“Tumeona mafanikio ya uhifadhi yanaongezeka, lakini sasa ni wakati wa kuhakikisha mafanikio hayo yanagusa moja kwa moja maisha ya wananchi na miradi isisimamiwe kwa mazoea lazima iakisi matokeo halisi,” amesema DC Sitta na kuongeza kuwa,
“Tusiruhusu mapato yatutumike vibaya. Wananchi wanapaswa kuona matokeo halisi,”
Ametoa wito wa kuwepo kwa mfumo madhubuti wa uwazi na taarifa kwa wananchi ili kila hatua ya matumizi ya fedha iwe wazi, jambo linalolenga kujenga imani na kuondoa migogoro ya kimaamuzi.
Wajumbe wa Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya Idodi na Pawaga (MBOMIPA) wakiwa katika kikao cha uwasilishwaji wa taarifa ya maendeleo ya jumuiya hiyo kwa mwaka 2024/2025 kilichofanyika leo, Desemba 19, 2025, katika ukumbi wa Chuo Huria cha Tanzania, Manispaa ya Iringa. Picha na Christina Thobias.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa MBOMIPA na wadau mbalimbali wa uhifadhi, ikiwemo mashirika ya kimataifa, taasisi za elimu na wawekezaji wa utalii, ili kuongeza ujuzi, teknolojia na rasilimali za kukabiliana na changamoto za ujangili na uharibifu wa mazingira.
Katibu wa MBOMIPA, Hassan Balama, amesema mapato ya jumuiya yameongezeka kutoka Sh64 milioni mwaka 2022/2023 hadi Sh700 milioni mwaka 2024/2025.
Mgao wa fedha kwa vijiji pia umeongezeka kutoka Sh30 milioni hadi Sh258 milioni, na kusaidia kuboresha huduma za afya, shule, miundombinu, ajira kwa vijana kama askari wa vijiji wa wanyamapori, na kutoa bima za afya kwa kaya 105.
“Mapato haya yametuwezesha kuboresha huduma za afya, shule, miundombinu na kuajiri vijana zaidi ya 50 kama askari wa vijiji wa wanyamapori na tumetoa bima za afya kwa kaya 105, jambo ambalo limeongeza usalama wa familia na ustawi wa kijamii,” amesema Balama.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya Idodi na Pawaga (MBOMIPA), Jonas Mkusa, akizungumza na viongozi mbalimbali wakati wa kikao cha uwasilishwaji wa taarifa ya maendeleo ya jumuiya hiyo kwa mwaka 2024/2025 kilichofanyika leo, Desemba 19, 2025, katika ukumbi wa Chuo Huria cha Tanzania, Manispaa ya Iringa. Picha na Christina Thobias.
Balama amesema mafanikio makuu yametokana na utalii wa wanyamapori na uwindaji wa picha, jambo ambalo limeongeza ustawi wa kijamii na kuelimisha jamii kuhusu uhifadhi. Hata hivyo, amebainisha changamoto zinazohitaji dharura, zikiwemo kupungua kwa fedha za utalii kutoka serikalini, ucheleweshaji wa malipo, ukosefu wa vitendea kazi, na migongano kati ya binadamu na wanyamapori, hususani tembo.
Wajumbe wa MBOMIPA walisisitiza kuwa uwazi na ushirikiano wa viongozi wa vijiji, kata na halmashauri ni muhimu kuhakikisha mapato yanagusa maisha ya wananchi moja kwa moja. Shaban Kodi wa kijiji cha Mbuyuni, Pawaga, amesema:
“Tunahitaji kuona mapato yanayopatikana kupitia utalii yanagusa maisha ya wananchi moja kwa moja, siyo tu kuhifadhi wanyamapori bila faida kwa jamii.”
Amina Malinzanga, mwakilishi wa Idodi, alisema uwazi ni msingi wa kuondoa hofu ya mapato kupotea au kutumika vibaya, na kuongeza kuwa mbinu za kisasa za usimamizi na utawala bora zinapaswa kuimarishwa kudhibiti changamoto za ujangili na migongano kati ya binadamu na wanyamapori.