‘Elimu ya historia itolewe kwa ubunifu, teknolojia’

Dodoma. Chama cha Wanahistoria Tanzania (HAT) kimetakiwa kusambaza elimu, utafiti na ubunifu wa kihistoria nchini badala ya kuuacha kwenye makaratasi bila jamii kunufaika nao.

Wito huo umetolewa leo Ijumaa Desemba 19, 2025 na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Shirika la Makumbusho ya Taifa, Revocatus Bugumba kwenye mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika jijini Dodoma.

Bugumba amesema kuwa Tanzania imejenga uhusiano wa kimataifa kupitia matukio ya kihistoria na urithi wa kiutamaduni, hatua iliyochangia kwa kiasi kikubwa maendeleo chanya ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.

Amesema uendelezaji wa historia unachukua nafasi muhimu katika kuimarisha mahusiano ya kimataifa.

 “Tukifanya tafiti ni muhimu zirudi kwa jamii husika kwa sababu ni kumbukumbu ya alama na utambulisho wao, pia katika kupambana katika kipindi hiki cha utandawazi na mabadiliko ya teknolojia ili historia iendelee kuwa utambulisho wa Taifa,” amesema.

Msomi huyo amesema yote yakiwezekana, inasaidia kujenga umoja wa kweli na kuhamasisha kizazi kijacho kiweze kuipenda historia yao,” amesema Bugumba na kuongeza;

“Hivi sasa kuna somo la historia ya Tanzania na maadili linalofundishwa shuleni ambalo ni jambo jema ili watoto wathamini walikotoka na waweze kuendana na teknolojia.”

Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Ali Mkubwa amesema kumekuwa na upotoshaji wa baadhi ya taarifa za historia nchini, hivyo ni lazima kufanyika utafiti wa kina ili kuboresha maeneo ya historia.

Dk Mkubwa amesema ni jukumu la HAT kuhakikisha wanafanya utafiti wa kutosha katika maeneo ya kihistoria nchini na kuja na taarifa sahihi zitakazoelimisha Watanzania kuhusu historia ya maeneo yao.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha wanahistoria nchini, Profesa Maximillian Chuhila amesema historia ni nembo ya Taifa na urithi wa utamaduni wenye kuitambulisha Tanzania, hivyo ni muhimu watu wakaijua.

Profesa Chihila amesema kila Taifa duniani lina historia yake, hivyo Watanzania ni lazima wajivunie historia yao ambayo ni urithi na utambulisho kila wanapokwenda.

Ameipongeza Serikali kwa kuanzisha somo la Historia ya Tanzania na maadili kwa wanafunzi kwani itasaidia vijana wengi kujifunza na kuifahamu historia ya nchi yao na kuachana na kuiga utamaduni wa kigeni.