Fainali Mapinduzi Cup 2026 kuchezwa Pemba

WAKATI michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 ikitarajiwa kuanza Desemba 28, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex kisiwani Unguja, imeelezwa kwamba fainali itapigwa Pemba.

Hayo yamesemwa na Katibu Kamati ya Kombe la Mapinduzi 2026, Rashid Said Suleiman alipozungumza na waandishi wa habari leo Desemba 19, 2025.

Suleiman amesema kabla ya kuchezwa fainali hiyo Januari 13, 2026 kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba, litafanyika tukio la uzinduzi wa uwanja huo uliofanyiwa maboresho makubwa.

“Fainali kama kawaida imekuwa ikichezwa Januari 13 kila mwaka na safari hii itafanyika Pemba kwenye Uwanja wa Gombani.

“Tunamshukuru Rais wa Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi kwa kuufanyia maboresho uwanja wa Gombani ambao umekuwa wa kisasa zaidi kama alivyofanya Uwanja wa New Amaan Complex ambao leo hii mechi kubwa za kimataifa zinachezwa hapa Zanzibar,” amesema Suleiman.

MAPI 01

Katika hatua nyingine, Suleiman amesema michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 itashirikisha timu 10 ambapo hatua ya makundi na nusu fainali, mechi zake zote zitachezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja, kisha fainali ndiyo itapigwa Gombani.

Hii itakuwa ni mara ya pili mfululizo fainali ya michuano hiyo kuchezwa Uwanja wa Gombani baada ya Kombe la Mapinduzi 2025 kufanyika hapo kuanzia hatua za mwanzoni hadi mwisho ikishirikisha timu za taifa ambapo Zanzibar Heroes ilibeba ubingwa kwa kuichapa Burkina Faso mabao 2-1.