Kabla ya kurudishwa kikosini Yanga, Pedro amwekea mtego Yao

WAKATI beki wa kulia Yao Kouassi akirejea uwanjani muda mfupi kabla ya kufunguliwa dirisha dogo la usajili Tanzania, inadaiwa benchi la ufundi chini ya Kocha Pedro Goncalves likishirikiana na uongozi una mpango wa kumtumia nyota huyo katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026.

Inaelezwa kocha Pedro na mabosi wa Yanga wanataka kuona kama beki huyo wa kulia raia wa Ivory Coast yupo fiti kiasi gani kabla ya kuamua kumrejesha katika kikosi hicho baada ya awali kumchomoa katika mfumo kutokana na kuwa majeruhi wa muda mrefu.

Michuano ya Mapinduzi inatarajiwa kuanza rasmi Desemba 29 ikishirikisha klabu 10, ikiwamo mbili zitakazotangazwa baadae sambamba na nane zilizotangazwa awali ambazo ni Yanga, Simba, Azam FC, Singida Black Stars, Fufuni, Mlandege, URA ya Uganda na KVZ.

Chanzo cha kuaminika kutoka Yanga kililiambia Mwanaspoti, licha ya kufahamika Yao ana hesabu siku kuingizwa katika mfumo wa usajili wa timu hiyo, lakini benchi la timu hiyo na  uongozi una mpango kwanza wa kumtumia kupitia Mapinduzi ili kumtengenezea utimamu wa mwili.

“Siyo kumrudishia utimamu tu bali mpango ni kuona ni namna gani anarudi  katika ushindani na kumuonyesha kocha, Yao ni mchezaji wa aina gani na ni namna gani anaweza kuisaidia timu,” chanzo hicho kilisema na kuongeza;

“Mchezaji mwenyewe anaonyesha uhitaji wa kupata mechi za mashindano ili arejeshe hali ya utimamu baada ya kukaa nje kwa muda mrefu na kama unavyoona mazoezini ni mchezaji ambaye ana juhudi sana.”

Chanzo hicho kilisema mchakato wa kumsajili Yao utategemeana na kile atakachokionyesha katika  michuano hiyo ambayo itatumiwa na wachezaji wengi ambao hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara kuonyesha uwezo wao kabla ya dirisha kufungwa ili kujua ni wangapi watapunguzwa na wangapi wataendelea kusalia Yanga.

“Mapinduzi sio kwa ajili ya beki huyo pekee, pia kuna wachezaji hawajapata nafasi ya kucheza tangu msimu umeanza ni wakati wao kuonyesha ni kwa nini wanastahili kuendelea kubaki Yanga au waweze kutolewa kwa mkopo kwenda timu nyingine kupisha nyota wataofaa kwa ushindani.”

Hivi karibuni Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe akizungumzia juu ya mchakato wa beki huyo aliwataja makocha, Pedro Goncalves na Kocha wa Utimamu wa miili, Chyna Mokaila kuwa ndio wataamua hatma ya beki huyo.

“Yao tunachosubiri sasa hivi ni ripoti kutoka kwa kocha wa utimamu wa mwili. Mchezaji ambaye ametoka katika majeraha ni ngumu mno kumkadiria kuwa, akishapona atarudi. Ikituambia mchezaji huyo amekamilika kwa asilimia zote, kocha atakuwa na namna yake ya kumchunguza Yao kuangalia ubora wake umefika wapi.

“Halafu yeye anatugea sisi mapendekezo yake, sasa hivi mnaweza kumuingiza katika usajili, nitamtumia. Amefika katika kiwango anachohitaji yeye tumuingize kwenye usajili au tumuache aendelee kufanya naye mazoezi au tumtoe kwa mkopo apate muda wa kucheza. Yote yanaweza kutokea hayo,” amesema Kamwe.