Kilimo cha kuokoa maisha kilivyosaidia wengi

Bahi, Dodoma. Tatizo la ukosefu wa damu miongoni mwa wanawake wajawazito katika wilaya za Bahi na Chamwino mkoani Dodoma limeanza kupata ufumbuzi, baada ya kuanzishwa kwa mradi wa lishe, unaolenga kuongeza upatikanaji wa damu kwa njia ya chakula.

Suluhu hiyo imetokana na utekelezaji wa mradi wa Lishe Yangu Afya Yangu unaoendeshwa na taasisi ya Save the Children kwa kushirikiana na Serikali, ukihamasisha matumizi ya mbogamboga na viazi damu (beetroot) miongoni mwa wanawake wajawazito na wanaonyonyesha.

Mbali na matumizi ya dawa za kuongeza damu, mradi huo umewezesha wanawake kujifunza kilimo cha bustani na matumizi sahihi ya vyakula vyenye virutubisho, hatua inayochangia afya na ustawi wa mama na mtoto.

Mmoja wa wanufaika wa mradi huo, Meleya Nyambuya amesema matumizi ya mbogamboga na viazi damu yamekuwa mkombozi wa afya yake wakati wa ujauzito, huku yakimpatia fursa ya kujiongezea kipato.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Desemba 19, 2025, Nyambuya amesema licha ya viazi damu kumsaidia kuongeza damu bila kutumia dawa, pia amekuwa akiuza mazao hayo na kupata fedha za kugharamia mahitaji ya nyumbani na maandalizi ya kujifungua.

“Nilikuwa na changamoto ya upungufu wa damu wakati wa ujauzito, lakini nilipoanza kutumia viazi damu hali yangu ilibadilika. Nilipopimwa na wataalamu waliniambia wingi wa damu yangu uko sawa,” amesema.

Ameeleza kuwa Save the Children ilimpatia mafunzo ya kuanzisha bustani ya mbogamboga pamoja na mbegu za viazi damu, ambavyo alivipanda na kuvitumia kama chakula na kinywaji.

“Walitufundisha namna ya kulima viazi damu na jinsi ya kuvitumia. Majani yake tunapika kama mboga na viazi vyake tunasaga na kunywa kama juisi. Viliniongezea damu na hadi ninajifungua nilikuwa na damu ya kutosha,” amesema.

Kwa upande wa kipato, Nyambuya amesema huuza kilo moja ya viazi damu kwa Sh3,000, fedha zilizomwezesha kununua samani za ndani na kugharamia mahitaji muhimu wakati wa kujifungua.

Naye Victoria Sway amesema alikumbwa na tatizo la upungufu wa damu alipokuwa mjamzito, hali iliyomlazimu kupata ushauri kutoka kwa wahudumu wa afya jinsi ya kutumia vyakula vyenye virutubisho ikiwemo viazi damu.

Mnufaika wa mradi wa lishe yangu afya yangu unaotekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la Save the Children, kutoka Kijiji cha Mundemu Wilayani Bahi, Meleya Nyambuya akionyesha kiazi damu alicholima kwenye bustani yake. Kiazi hicho kinatumika kuongeza damu kwa akina mama wajawazito. Picha na Rachel Chibwete

“Nilipoanza kliniki nilikuwa na wingi wa damu asilimia tano, ambacho ni kidogo kwa mjamzito. Baada ya kutumia viazi damu, kiwango cha damu kilipanda hadi asilimia 12 na niliweza kujifungua salama,” amesema Sway.

Muuguzi wa Kituo cha Afya Mundemu, Anna Mokiwa, amesema viazi damu vimekuwa msaada mkubwa kwa wajawazito, hasa kwa wale wanaoshindwa kumeza vidonge vya kuongeza damu kutokana na harufu au madhara madogo kama kichefuchefu na kutapika.

Amesema tangu kuanza kwa matumizi ya zao hilo, kumekuwa na mabadiliko makubwa katika viwango vya damu kwa wajawazito wanaohudhuria kituo hicho.

“Kuanzia Januari hadi Desemba 2025, wanawake wengi tunaowapokea wana wingi wa damu kuanzia asilimia tisa, tofauti na miaka ya nyuma ambapo wengi walifika wakiwa na kiwango cha asilimia tano hadi saba. Matumizi ya viazi damu yameleta manufaa makubwa,” amesema Mokiwa.

Mhudumu wa afya ngazi ya jamii Mundemu, Veronica Mwigalawa, amesema mradi wa Lishe Yangu Afya Yangu umeleta matokeo chanya siyo kwa wajawazito pekee bali kwa jamii kwa ujumla.

Hata hivyo, amesema bado kunahitajika elimu zaidi, kwani baadhi ya wananchi wanadai viazi damu vina harufu mbaya.

“Tunaendelea kutoa ushauri wa kuchanganya viazi damu na ubuyu au kuweka sukari kidogo ili kuboresha ladha. Wengi wanaofanya hivyo hufurahia kinywaji hicho,” amesema Mwigalawa.

Kwa upande wake, Mratibu wa mradi huo Mariam Mwita, amesema lengo la mradi huo ni kuboresha uhakika na usalama wa chakula na lishe mkoani Dodoma.

Amesema kutokana na mafanikio yaliyopatikana, shirika hilo limeanza kampeni ya kugawa mbuzi wa maziwa na kuanzisha bustani za mbogamboga kwa kutumia mbinu zinazozingatia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Kwa kushirikiana na Serikali, tunahamasisha matumizi ya maziwa ya mbuzi na chakula mchanganyiko ili kujenga kinga ya mwili na kupunguza idadi ya wananchi wanaohitaji huduma za hospitali,” amesema.

Kwa mujibu wa Mwita, hadi sasa Save the Children imegawa mbuzi 1,741 kwa walengwa ambao ni wajawazito na wenye watoto chini ya umri wa miaka mitano, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa maziwa na kuboresha lishe ya watoto katika jamii.