Mpogolo Awasisitiza Madiwani Ilala Kushirikiana na Serikali za Mitaa Kutatua Kero za Wananchi

 

Na Mwandishi wetu 

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amewataka madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kufanya kazi kwa kushirikiana na Watendaji pamoja na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ili kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Mpogolo aliyasema hayo wilayani Ilala wakati wa kufunga mafunzo ya siku tatu kwa madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, yaliyolenga kuwajengea uwezo katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Nawaomba madiwani wangu wa Halmashauri ya Jiji kuwa kiunganishi kati yenu, Watendaji na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa katika kutatua changamoto za wananchi, ili kwa pamoja tumsaidie Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema Mpogolo.

Aliwataka madiwani kushuka hadi ngazi ya mtaa kwa kushirikiana na Watendaji pamoja na Wenyeviti, ambako ndiko kero nyingi za wananchi zilipo, ikiwemo kuitisha vikao vya utatuzi wa kero na mikutano ya hadhara.

Mpogolo alisisitiza kuwa mafunzo hayo yanapaswa kuwa na tija kwa wananchi kwa kuwahudumia kwa ufanisi katika maeneo yao. Alisema kiongozi anayefahamu changamoto za wananchi hawezi kuona ni mzigo kuwahudumia.

Aliwataka madiwani kwenda kutatua kero za wananchi katika kata, mitaa na maeneo yao kwa vitendo, akibainisha kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo kuhusu uendeshaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Wakati huohuo, aliwataka madiwani wa Ilala kusimamia kwa karibu ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ili Serikali iweze kufikia malengo yake ya kuongeza mapato.

Kwa upande mwingine, Mpogolo aliwasisitiza madiwani kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali Kuu ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokusudiwa.