Sababu kesi ya kuporomoka jengo la Kariakoo yakwama mara ya nane

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa tena kusikiliza maelezo ya mashahidi na vielelezo (Commital Proceedings) katika kesi ya kuua bila kukusudia inayowakabili wafanyabiashara sita wakiwemo wamiliki wa jengo lililoporomoka Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo.

Kesi hiyo imeshindwa kuendelea kutokana na Jamhuri kubaini baadhi ya nyaraka muhimu katika kesi hizo hazijapandishwa katika mfumo wa mahakama.

Hii ni mara ya nane kwa Jamhuri kushindwa kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo washtakiwa hao, tangu upelelezi wa kesi hiyo ulipokamilika Septemba 11, 2025,  kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kuchukua muda kuchapisha nyaraka za kesi hiyo na kuzipandisha katika mfumo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ambao wote ni wakazi wa Dar es Salaam ni Leondela Mdete (49) mkazi wa Mbezi Beach, Zenabu Islam (61), mkazi wa Kariakoo na Ashour Awadh Ashour (38) mkazi wa Ilala.

Baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki wa watu 31 waliofariki kutokana na jengo kuporomoka mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, wakiwa nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kesi ya kuua bila kukusudia inayowakabili wafanyabiashara sita kuahirishwa. Picha na Hadija Jumanne

Wengine ni Soster Nziku (55) mkazi wa Mbezi Beach, Aloyce Sangawe (59) mkazi wa Sinza na Stephen Nziku (28) mkazi wa Mbezi Beach.

Hata hivyo, siku hiyo upelelezi ulipokamilika, upande wa mashtaka uliomba tarehe fupi kwa ajili ya kutajwa na kuangalia iwapo nyaraka muhimu za kesi hiyo zimeshasajiliwa Mahakama Kuu.

Ombi hilo lilikubaliwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini anayesikiliza kesi hiyo na kuiahirisha hadi Septemba 18, 2025.

Kesi hiyo ilipotajwa Septemba 18, 2025 Jamhuri ilidai haijamaliza kuchapa nyaraka kwa sababu kesi hiyo ina mashahidi wengi.

Kutoka na hali hiyo, kesi hiyo iliahirishwa hadi Oktoba 9, 2025 na siku hiyo ikadaiwa wanachapa jalada la kesi na kuomba ahirisho fupi, ndipo mahakama ikapanga Novemba 5, 2025.

Novemba 5, 2025 kesi haikuendelea na badala yake iliahirishwa hadi Novemba 17, 2025.

Ilipotwa Novemba 17, 2025, washtakiwa hao hawakusomewa maelezo wala vielelezo kutokana na Jamhuri kutomaliza kuingiza nyaraka kwenye mfumo ndipo iliahirishwa hadi Novemba 27, 2025.

Baadhi ya washtakiwa wa kesi ya mauaji bila kukusudia inayomkabili Zenabu Islam (kulia) na Awadh Ashour (38) na wenzao wanne ambao hawapo pichani, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne

Novemba 27, 2025 kesi hiyo ilipoitwa Mahakama kuwa Jamhuri ilidai kuwa tayari wameshasajili nyaraka muhimu kuhusiana na kesi hiyo Mahakama Kuu na hivyo wanasubiri muongozo wa mahakama.

Hakimu Mhini aliahirisha kesi hiyo na kuipangia siku mbili mfululizo, ambapo Jamhuri ilitakiwa kuja kuwasomea maelezo hayo.

Hata hivyo, Desemba 3, kesi hiyo haikuendelea kutokana na Hakimu Mhini kuwa na majukumu mengine ya kikazi na hivyo iliahirishwa kwa hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Gwantwa Mwankuga hadi Desemba 18 na Desemba 19, 2025.

Jana vilevile, haikuendelea kutokana kesi hiyo kuchelewa kuanza na hivyo hakimu akashauri wasomewe maelezo hayo leo, Desemba 19, 2025.

Leo Ijumaa, Desemba 19, 2025, Wakili wa Serikali, Gloria Kilawi ameiambia mahakama kuwa kesi hii iliitwa lakini pia baadhi ya nyaraka hazijaingizwa katika mfumo wa mahakama kwa ajili ya kusomwa.

“Tulikuwa tunafanya uhakiki wa nyaraka kwenye mfumo, lakini kwa bahati mbaya tumebaini baadhi ya nyaraka hazijapandishwa na tumeshindwa kuziona, kwa sababu hiyo tunaomba tupangiwe tarehe fupi ili tuweze kuziingiza katika mfumo,” alidai wakili wa Serikali.

Hakimu Mhini baada ya kusikiliza maelezo hayo, alikubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Desemba 30, 2025.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa Mahakamani hapo Novemba 29, 2024 na kusomewa mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa yao kinyume na kifungu 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Kwa pamoja wanadaiwa Novemba 16, 2024 katika mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, washtakiwa hao isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha vifo vya watu 31.