…….
Na Daniel Limbe, Geita
TANZANIA ikiwa ni miongoni mwa nchi ambazo bado zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa ajira kwa vijana wake, serikali imeanza kuweka mikakati ya kuimalisha sekta ya kilimo biashara ili kukuza pato la mtu mmoja mmoja, kaya na taifa kwa ujumla.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza ruzuku ya mbegu, mbolea, matrekta, uchimbaji mabwawa kwaajili ya kumwagilia pamoja na kuongeza stadi za kilimo kwa wakulima.
Ili kufikia azma hiyo, suala la stakabadhi za ghala limetajwa kuwa mwarobaini wa kukuza uchumi wa wakulima hasa vijana wa mkoa wa Geita ambao awali walikuwa wakikabiliwa na uhaba wa masoko ya uhakika.
Hata hivyo Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) imewataka wakulima kuacha kilimo cha mazoea chenye uzalishaji wa kujikimu badala yake wazingatie kilimo biashara ili kujikwamua na lindi la umaskini wa kipato kwa madai kilimo kinalipa.
Mkurugenzi mkuu wa COPRA Tanzania, Irene Mlola, ametumia fursa hiyo kumkabidhi tani 93 za mbegu bora za Alizeti mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigela, ikiwa ni ishara ya mpango mkakati mpya wa uzalishaji wa zao hilo kwa wakulima wa mkoa huo.
Aidha tani hizo zenye thamani ya shilingi milioni 470 zinatazamiwa kuchochea uzalishaji wa Alizeti bora na kuwa na mbegu hai tani 20,000 katika msimu wa 2025/26.
Amesema kutokana na maombi mbalimbali ya wakulima na viongozi wa umma kusaidia upatikanaji wa mbegu za Alizeti pamoja na wanunuzi wa uhakika katika mkoa huo, COPRA imeamua kutoa mbegu hizo ili kuwavutia wakulima kuzalisha kwa wingi na kuinua uchumi wao.
Mlola, amesema iwapo mbegu hizo zitapelekwa haraka kwa wakulima na kuzalishwa kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa kilimo, serikali inakusudia mkoa wa Geita kushika nafasi ya pili kitaifa kwa mavuno bora yatakayosaidia Uchumi wa Mtu, Kaya na Taifa kwa ujumla.
Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigela, ametumia fursa hiyo kuishukuru serikali kwa kutekeleza azma ya kuwakomboa wakulima kiuchumi na kwamba ili Tanzania iweze kupiga hatua kubwa katika mikakati ya viwanda, hakuna budi kuongeza uzalishaji wa mali ghafi zitokanazo na kilimo.
Amesema takribani aslimia 80 ya watanzania wanajihusisha na kilimo, hivyo ndiyo sekta pekee inayoweza kusaidia uchumi wa wananchi na ndiyo maana serikali imeamua kuweka mkazo na kutenga bajeti kubwa ili watanzania waweze kunufaika zaidi.
Kadhalika ameagiza maofisa ugani wote mkoani humo kuondoka maofisini ili kwenda kuwatembelea na kuwashauri wakulima namna bora ya kuzalisha kwa tija badala ya jamii kuendelea na kilimo cha mazoea.
Baadhi ya wakulima mkoani humo, Verediana Nyambibo na Masunga Mihayo, wameishukuru serikali kupitia COPRA kwa kutambua thamani ya wakulima katika pato la taifa na kwamba mfumo wa stakabadhi za ghala pamoja na uzalishaji wa alizeti utasaidia kurejesha Imani ya kilimo kwa jamii.
Kikao cha wadau wa kilimo cha mazao ya Choroko, Dengu, Mbaazi na Alizeti kimewahusisha baadhi ya wakuu wa wilaya za mkoa huo, Wabunge, wenyeviti wa halmashauri, wakurugenzi wa halmashauri, viongozi wa Amcos, Vyama Vikuu vya ushirika wa mazao, wauzaji wa Pembejeo pamoja na wakulima 40 kutoka kila wilaya za mkoa wa Geita.
