Simba, Yanga kuanza hivi Mapinduzi Cup 2026

KLABU kongwe za Simba na Yanga zimepangwa kuanza vita ya kuwania Kombe la Mapinduzi 2026 Januari 3 na 4, wakati pazia la michuano hiyo likifunguliwa na watetezi Mlandege dhidi ya Singida Black Stars Desemba 28, 2025.

Simba ambayo jioni hii imemtangaza kocha mkuu mpya, Steve Becker kutoka Stellenbosch ya Afrika Kusini, imapangwa kundi B na itaanza kucheza na Mwembe Makumbi Saa 2:15 usiku, ikiwa ni mechi ya pili kwa siku hiyo, baada ya kutanguliwa na Singida Black Stars itakayocheza dhidi ya URA ya Uganda mapema Saa 10:15 jioni.

Simba iliyotwaa mara nne taji hilo kwa miaka ya 2008, 2011, 2015, 2022, itashuka tena dimbani kuhitimisha mechi hatua ya makundi kwa kucheza na Fufuni ya visiwani Zanzibar Januari 5, 2026.

Kwa upande wa Yanga iliyochukua taji hilo mara mbili mwaka 2007 na 2021, imepangwa kundi C, ambapo itaanza kucheza dhidi ya KVZ ya Zanzibar Januari 4, 2026, kisha kuhitimisha kwa kupambana na TRA United zamani Tabora United, Januari 6, 2026.

Licha ya mechi hizo kuanza Desemba 28, 2025, kutakuwa na mapumziko Desemba 30, 2025 ili kutoa fursa kwa Watanzania kushuhudia Taifa Stars ikicheza mechi ya mwisho ya hatua ya makundi katika fainali za AFCON 2025 dhidi ya Tunisia huko  Morocco.

Pia, kwa mujibu wa Katibu wa Kamati ya Kombe la Mapinduzi 2026, Rashid Said Suleiman, amesema mapumziko hayo yataendelea hadi Januari Mosi, 2026, kwa lengo la kupisha Sikukuu ya mwaka mpya.

Awali, ilidaiwa huenda Yanga na Simba zisingeshiriki michuano hiyo itakayohitimishwa Januari 13, 2026, ingawa kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) na Kombe la Mapinduzi, Mohamed Kabwanga, hakuna kitu hicho.