Sugu ataja suluhisho mgogoro wa wasanii, mashabiki

Dar es Salaam. Msanii wa Hip-Hop nchini na mwanasiasa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu, ametoa ya moyoni dhidi ya mgogoro unaoendelea nchini baina ya wasanii na mashabiki wao.

Sugu amezungumza hayo leo Alhamisi, Desemba 18, 2025, alipozungumza na Mwananchi, baada ya mjadala unaoendelea baina ya pande hizo mbili, ambao umefikia hatua ya kumfanya hadi Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, kuingilia kati kuwatetea wasanii.

Jana, Jumatano Desemba 17, 2025, alipokuwa ziarani mkoani Songwe, Dk Mwigulu alizungumzia mvutano huo unaoendelea akisema kuimba kwenye kampeni ni sehemu ya ajira kwa wasanii.

“…mtu anakaa huko sijui kwenye nchi yake ameshapata uraia kisa anaongea Kiswahili, mwingine amehifadhiwa huko. Eti anawaambieni wasanii wakataeni walienda kwenye kampeni za CCM. Ajira ya msanii ni Sanaa, unataka mtu aache ajira yake,” alisema Dk Mwigulu na kuongeza:

“Nani kawaambia wachezaji wanaocheza Manchester ni mashabiki wa Manchester? Nani kawaambia watu wanaocheza Simba ni mashabiki wa Simba? Uchezaji ni ajira yao. Msanii akienda kuimba yeye pale yupo kazini, yupo kwenye ajira yake. Tunahangaika vijana wapate, wewe unasema wakatae fursa ya kupata fedha.”

Kauli ya Dk Mwigulu kuwatetea wasanii ni sawia na ile ya Mkurugenzi wa EFM Radio, Francis Ciza ‘Majizzo’, aliyejitokeza kuwaombea wasanii msamaha huku akimtaka Sugu kupaza sauti.

Sugu akizungumza katika mahojiano na Mwananchi leo, ameeleza walipofikia na njia za kujinasua na mvutano huo.

Sugu aliyewahi kuwa Mbunge wa Mbeya Mjini kupitia Chadema, akiwa miongoni mwa wadau wakubwa wa mjadala huo, ameweka msisitizo kuwa chanzo cha mgogoro si wasanii kushiriki kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025 bali ni wasanii kushindwa kupaza sauti kuhusu matatizo ya jamii.

“Hii issue haihusiani kabisa na kushiriki kampeni za vyama. Watu wanasahau mimi niliwahi kusimama na kumpendekeza Kikwete pale Jangwani, baada ya kupitishwa mbele ya Mkapa.

“Nilivyoitwa pale nilisema kabisa mimi siyo CCM, John Komba akaniambia ni kweli hili tunafanya kwa ajili ya nchi. Kikwete wakati ule alikuwa amebeba matumaini ya Watanzania wengi na alijiweka kama kijana. Hapo ndiyo ukawa mwanzo wa Bongo Fleva kutumika kwenye kampeni za CCM,” amesema Sugu.

Amesema kipindi hicho si yeye pekee aliyeshiriki kampeni hizo, hata Professor Jay aliwahi kushiriki.

“Hii ishu ni sasa hivi CCM inafanya nini, inaleta madhara gani kwa nchi ambayo yanawaletea shida wananchi. Wananchi wanataka kusemewa, wamewapa wasanii sauti.

“Matarajio ya wananchi ni kuona kama mfumo wa vyama vya siasa umefutwa, maana yake wananchi sasa wanatarajia kusikia sauti nyingine, na sauti wanazotarajia kuziona zenye nguvu ni za wasanii,” amesema Sugu.

Amesema mtu akipata umaarufu unaotokana na sapoti ya wananchi, basi anakuwa mali ya umma.

“Ukifanikiwa kupitia sanaa kwa ujumla, wewe ni mali ya umma, kwa sababu wao ndiyo wamekufikisha pale. Kwa hiyo wanakutarajia usimame nao, sauti yako isikike pale ambapo jamii inahisi inahitaji kusemewa.

“Tumekuwa na mambo mengi sana. Siyo sasa, tangu nyuma. Roma hakutekwa wakati wa Samia, alitekwa wakati wa Magufuli, na tukakemea, wasanii wakatukera kwa kutokusema. Haya mambo hayajaanza leo,” amesema Sugu.

Amesema kadri nchi inavyozidi kuingia kwenye magumu, ndivyo wasanii wanavyozidi kukaa mbali na umma na badala yake wanakuwa upande wa watesi.

“Nchi ipo kwenye majonzi, msanii anachapisha picha yupo kwenye shooting ya video. Yaani hamna hata utu. Mtu aone aibu. Unaweza ukaona kwa nini wananchi wanakuwa na hali waliyonayo sasa, sababu wanawadai wasanii.

“Hawa walikuja wakiwa maskini wanapotoka. Umma ukawapa sapoti wakanyanyuka. Wasanii wamelikosea taifa, walichotakiwa ni kuomba radhi, siyo kubeza,” amesema.

Mkali huyu wa vibao kama Hayakuwa mapenzi, Mtit’ na Taita amesema uzito wa jambo hilo umeendelea kuonekana baada ya Waziri Mkuu kulizungumzia.

“Waziri Mkuu yupo barabarani badala ya kuwasilisha masuala ya kitaifa, anaanza kutetea wasanii ambao wananchi wamewakataa,” amesema.

Mbali na hayo, Sugu ameendelea kusema nchi imefika katika mgogoro huo wa wasanii na mashabiki kwa sababu ya ushamba wa wasanii.

“Umepata unaanza kudharau watu wanaokuzunguka. Wasanii wamelikosea taifa, wanatakiwa kuomba radhi wao wenyewe, siyo kuombewa na Waziri Mkuu wala Majizzo.

“Kitu cha msingi ambacho tunapaswa kuwa nacho makini ni kuhakikisha kiwanda cha muziki hakifi. Sisi hatukujenga watu, tulijenga ‘industry’. Tutahakikisha haifi, ikibidi tuanze upya. Hii industry ni endelevu. Hawa ambao wameibagaza na kuifanyia mabaya yote, kama wameona haiwafai waendelee huko,” amesema.

Sugu amewataka wasanii waache viburi, kwani tayari wameikosea jamii.

“Hili ni tatizo la Tanzania kwenye mambo mengi, linapokea jambo, kila mtu anajua tatizo ni nini, lakini wanapambana kutengeneza simulizi tofauti.

“Siasa haiwezi kutatua. Ili tutatue matatizo yetu, ni lazima twende kwenye kiini kama taifa, siyo tu kwenye Bongo Fleva. Hii ni kwenye changamoto zote zinazotukabili kama taifa,” ameeleza Sugu.

Majizzo alisema kuna uwezekano kundi fulani la wasanii lilipitiliza au kujikwaa sehemu walipochagua upande wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

“Kwangu mimi naona ni msanii ambaye ameadhibiwa kwa kosa la kujitafutia riziki, kwa kosa la kwenda kutafuta kipato chake. Kumbuka hawa wasanii walikuwa kwenye majukwaa ya siasa, walikuwa wanalipwa, kwa hiyo mtu ameenda kujitafutia riziki, sisi tunamwadhibu.

“Kuna wakati wanakosea, wana maneno ya kukera, na kuna wakati wanapitiliza. Kibinadamu ni vizuri kukiri, mimi kama kaka, kama mshikadau wa sanaa, nawaombea radhi kwa niaba yao ili tasnia isonge mbele,” alisema Majizzo.