Mbarali. Wakati wakulima wa mazao ya chakula na biashara katika Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya, wakianza maandalizi ya msimu huu wa kilimo, imeelezwa kuwa ukosefu wa mvua za uhakika umesababisha kusuasua kwa soko la mbolea ya ruzuku.
Hali hiyo imetokana na wakulima wengi kushindwa kufanya maamuzi ya kununua mbolea mapema, wakisubiri mvua za uhakika ili kuepuka hasara.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa, Desemba 19, 2025, Wakala mkuu wa uuzaji na usambazaji wa mbolea Wilaya ya Mbarali, Kenneth Ndingo, amesema hali hiyo imewaathiri katika mzunguko wa fedha kutokana na kushuka kwa mauzo ya mbolea katika kipindi cha maandalizi ya msimu wa kilimo.
“Kimsingi nimeathirika sana. Nina zaidi ya mifuko 2,000 iliyohifadhiwa kwenye ghala, na uwekezaji huo nimechukua mkopo kwenye taasisi za kibenki ambao napaswa kurejesha muda ukifika,” amesema.
Kuhusu ukosefu wa soko la uhakika, amesema unasababisha mbolea kukaa muda mrefu bila kuuzwa, jambo linalokwaza mzunguko wa fedha na kuwa kikwazo katika kulinda mtaji na faida kwa wafanyabiashara.
Sehemu ya shehena ya mbolea iliyohifadhiwa kwenye ghala ikisubiri wateja. Picha na Hawa Mathias
“Tunaumia mbolea inapokaa muda mrefu mzunguko wa fedha unakuwa mgumu, na malengo niliyokusudia yameenda tofauti,” amesema.
Mchango wa mbolea ya ruzuku
Ndingo amesema wanapangiwa na Serikali sehemu ya faida na bei elekezi sokoni ambazo ni lazima wazifuate ili kutimiza matakwa ya kisheria.
“Hii mbolea ya ruzuku naagiza kwa Sh104,000 kwa kila mfuko, ambapo wakulima walio kwenye mfumo rasmi wanauziwa Sh79,000, lakini fedha ya juu kama wakala nalipwa na Serikali baada ya mzunguko kwa kila msimu husika,” amesema.
Naye msimamizi wa uuzaji na usambazaji wa mbolea ya ruzuku, Merania Mnyawami, amesema biashara imekuwa ngumu tofauti na miaka ya nyuma.
Aidha, ametaja changamoto nyingine kuwa ni kuwepo kwa shida ya mtandao kwa ajili ya kuwaingiza wakulima kwenye mfumo.
“Msimu ukichanganya kuna shida ya mfumo wa kielektroniki kupitia Mamlaka ya Mbolea Tanzania, unaohusisha kuingiza namba za ruzuku za wakulima ili kufanya mauzo, jambo ambalo hukwamisha shughuli kwa siku mbili hadi tatu na kuathiri mzunguko wa fedha,” amesema.
Amesema kutokana na changamoto hiyo wanaiomba Serikali kufanya maboresho ya mifumo ya kielektroniki kabla ya msimu wa mauzo kuchanganya, ili kurahisisha kazi.
Meneja wa Wakala Mkuu wa Uuzaji na Usambazaji wa Mbolea, Jonson Mwaiteleke, amesema kwa sasa wanazo takribani tani 120 za mbolea ambazo bado zinasubiri kupatiwa soko.
Mwaiteleke ameeleza kuwa katika msimu huu hali ni tofauti na msimu uliopita, ambapo wakulima wengi wamesita kununua mbolea wakisubiri kupatikana kwa mvua za uhakika.
Amesema hali hiyo imewaathiri kwa kiasi kikubwa wao kama wasambazaji, kutokana na kupungua kwa mauzo katika kipindi cha maandalizi ya msimu wa kilimo.
Mkulima wa zao la mpunga kutoka Kijiji cha Mswiswi, Wilaya ya Mbarali, Peter Fredy amesema wakulima kwa sasa wameshindwa kuanza ununuzi wa mbolea kutokana na kusuasua kwa mvua katika msimu huu wa kilimo.
“Tumekaa mguu sawa kusubiri mvua zinyeshe ili tuanze kukimbizana kununua mbolea za ruzuku. Kwa sasa ni vigumu, kwani matokeo ya kila mkulima ni kuangalia hali ya hewa ili kuanza uzalishaji,” amesema.
