Juhudi za kukabiliana na changamoto za matumizi ya nishati chafu, uharibifu wa mazingira na magonjwa yatokanayo na moshi wa kuni na mkaa zimepata msukumo mpya kufuatia uzinduzi wa Soko la Chakula la Stendi ya Msamvu, lililoanzishwa chini ya Mradi wa Mwanamke Shujaa unaotekelezwa na Coca-Cola Kwanza kwa kushirikiana na Oryx Gas Tanzania na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa mawasiliaano ya jamii Coca-Cola Kwanza, Salumu Nasoro alisema kuwa mradi huo unalenga kuwaokoa wanawake wanaojishughulisha na biashara ya mama lishe dhidi ya athari za kiafya na kimazingira zitokanazo na matumizi ya kuni na mkaa katika maeneo yao ya kazi.
Nasoro alisema kuwa kwa Mkoa wa Morogoro, wanufaika wa mradi ni wanawake 450, huku wanawake 150 wakitoka katika eneo la Msamvu.
Alifafanua kuwa mradi huo umejikita katika kuwawezesha wanawake kiuchumi na kiafya kwa kuwapatia mazingira salama na rafiki kwa mazingira ya kuendeshea shughuli zao za ujasiriamali.
“Mradi wa Mwanamke Shujaa unaweka mkazo katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, hususani gesi ya LPG, ili kupunguza magonjwa ya njia ya hewa, kulinda mazingira na kuongeza tija kwa wanawake wafanyabiashara,” alisema Nasoro.
Kupitia mradi huo, soko maalum la Msamvu limeanzishwa likiwa na vibanda 50 vya kisasa, vilivyopangika na salama, hatua inayowaondoa wanawake waliokuwa wakifanya biashara katika mazingira hatarishi kando ya barabara na maeneo yasiyo rasmi.
Aidha, mradi huo unatekeleza malengo yake kupitia mafunzo ya ujasiriamali na uendeshaji wa biashara, kuongeza fursa za kipato na ajira kwa wanawake pamoja na kuwapatia vitendea kazi vya kisasa na mazingira bora ya kufanyia kazi
Kwa upande wake, Balozi wa Nishati Safi Jenepha Mosha alisema matumizi ya gesi ya kupikia yanachangia kukuza uchumi wa kaya, kulinda mazingira kwa kupunguza ukataji miti, na kulinda afya ya wanawake ambao ndio waathirika wakubwa wa moshi unaotokana na kuni na mkaa.
“Nishati safi ni suluhisho la moja kwa moja la changamoto za kiafya na kimazingira. Wanawake wanapobadili mtindo wa kupikia, tunapunguza hewa chafu, tunahifadhi misitu na tunaboresha maisha,” alisema Mosha.
Katika kuunga mkono jitihada hizo, Oryx Gas Tanzania imetoa mitungi ya gesi yenye thamani ya shilingi milioni 11, hatua inayorahisisha upatikanaji wa nishati safi kwa wanawake wanufaika wa mradi huo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Mkuu wa Idara ya Viwanda na Biashara, John Kulunge alisema Manispaa imeingia ubia na wadau wa maendeleo ili kutatua changamoto ya matumizi ya nishati chafu ya kupikia, akisisitiza kuwa nishati safi ni ajenda ya kitaifa.
“Matumizi ya nishati safi ni kipaumbele cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kupitia nishati safi, tunaokoa misitu na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa,” alisema Kulunge.
Aliongeza kuwa mafunzo yaliyotolewa yameleta mabadiliko ya mtazamo kwa wanawake wanufaika, hasa baada ya kukabidhiwa vitendea kazi vya kisasa vinavyowezesha ufanisi na usalama katika biashara zao.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Morogoro, Khalid Matengo aliwataka wafanyabiashara wa chakula (mama lishe) katika eneo la Msamvu kutumia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa kuanzisha vikundi vya kijamii na kiuchumi.
