Wastaafu 50,000 kufikiwa na vitambulisho vya kielekroniki

Dodoma. Jumla ya wastaafu 50,000 wanaolipwa kupitia Hazina nchini kote wanatarajia kupatiwa vitambulisho vya kielektroniki katika kipindi kifupi, huku tayari 609 wa Jiji la Dodoma wameshakabidhiwa.

Mpango wa ugawaji wa vitambulisho kwa wastaafu ulianza mapema mwezi huu katika Jiji la Dodoma na unatarajiwa kuwaunganisha wastaafu wote nchini ifikapo mwisho wa Januari 2026, chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha, ili kufikia wastaafu wapatao 50,000.

Takwimu hizo zimetolewa leo, Ijumaa Desemba 19, 2025, na Mhasibu Mkuu Msaidizi wa Serikali wa Huduma za Mfuko Mkuu, Perfectus Killenza, wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya kazi hiyo kutoka Wilaya ya Dodoma Mjini, inayoendelea katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, Dodoma.

Killenza amesema vitambulisho hivyo vya kielektroniki ni salama, imara na vinaondoa changamoto zilizokuwepo awali kwa vitambulisho vya karatasi, ambavyo viliharibika kwa urahisi na kufanya taarifa zisomeke kwa shida.

 “Vitambulisho hivi vipya vitarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wastaafu wetu kwa kuwa taarifa zao zitasomeka kwa urahisi kwa njia ya kielektroniki, sambamba na kuongeza ulinzi na uhakika wa kumbukumbu zao,” amesema Killenza.

Mhasibu huyo amesema kuwa zoezi hilo limekuwa muhimu katika kuboresha taarifa za wastaafu waliofanikiwa kufika Ofisi za Hazina, jambo linalosaidia kuondoa changamoto ya baadhi ya wastaafu kutoweza kusomana vizuri.

Killenza amesisitiza kuwa wastaafu wote wa Wilaya ya Dodoma Mjini wanaohudumiwa na Hazina wanapaswa kufika katika Ofisi za Wizara ya Fedha wakiwa na nyaraka zao muhimu, ili kurahisisha kazi ya kuhakikiwa na kupatiwa vitambulisho vipya vya kielektroniki kwa muda uliopangwa.

Amesema kuwa utaratibu wa ugawaji wa vitambulisho utafanyika nchi nzima kuanzia Januari 2026, huku ratiba kamili itakayotolewa, lakini amesisitiza kuwa wanataka zoezi hilo lifanyike kwa haraka.

Kwa upande mwingine, amewakumbusha wastaafu wote kuwa huduma zote zinazohusiana na pensheni ni bure, hivyo wanapaswa kuwa waangalifu ili kuepuka udanganyifu na matapeli.

 ‘’Wastaafu wote wanaolipwa na Hazina ni muhimu kuepuka watu au makundi yanayodai kuwawezesha kupata huduma kwa malipo, kwa kuwa kufanya hivyo kunaweza kuwaweka kwenye mtego wa udanganyifu na kupoteza fedha zao,’’ amesema.

Mmoja wa wastaafu wanaonufaika na huduma hiyo, Selemani Ramadhani, amesema huduma hiyo ni nzuri, lakini aliomba iendelee kutolewa kwa wingi zaidi, ili kuwasaidia wastaafu au warithi wao kupata mafao yao kwa wakati unaotakiwa.

Selemani ameeleza kuwa uwepo wa vitambulisho vya kielektroniki unaweza kuwasaidia sana, kwani utunzaji wa vitambulisho vya karatasi kwa umri wao ulikuwa changamoto, na mara nyingine wastaafu walilazimika kuwa na nyaraka zaidi ya moja.

Kwa upande wake, Severina Kivangala amewahimiza wastaafu wengine nchini kujitokeza mara watakapoitwa, ili wapate huduma hizo.

Pia, ameomba Wizara ya Fedha kuanza kutoa huduma hizo mikoani, badala ya kuwalazimisha wastaafu kufika makao makuu ya kata.