Watatu kuifuata Taifa Stars leo

TIMU ya taifa, Taifa Stars jana Alhamisi imeondoka kambini jijini Cairo, Misri kwenda Morocco kwa ajili ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, huku mastaa watatu wa timu hiyo waliokuwa wamekwama jijini Dar es Salaam wakitarajiwa kuondoka leo kuifuata.

Wachezaji hao watatu waliokuwa wamekwama jijini Dar es Salaam kwa muda wote wakati wenzao wakiwa kambini Misri, bila kufahamika kilichowakwamisha ni kiungo Yusufu Kagoma, mshambuliaji Seleman Mwalimu ‘Gomez’ na beki Lusajo Mwaikenda wanaoondoka leo kwenda kuungana na timu.

Stars imepangwa Kundi C sambamba na Uganda ‘The Cranes’, Nigeria ‘Super Eagles’ na Tunisia ‘Eagles of Carthage’ na itaanza mechi zake Desemba 23 dhidi ya Nigeria kabla ya kuvaana na Uganda Desemba 27 kisha kumaliza mechi za kundi hilo na Tunisia Desemba 30.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kagoma alithibitisha safari hiyo kuanza leo, huku akishindwa kuweka wazi sababu zilizowafanya kuchelewa kuungana na wenzao walioondoka nchini mapema  karibu wiki mbili zilizopita na kucheza mechi mbili za kirafiki kabla ya kutua Morocco.

“Ni kweli tunaondoka kesho (leo) kuhusu kuchelewa kuungana na wenzangu sina majibu ninachofahamu natakiwa kuondoka leo tayari kwa ajili ya mashindano yaliyo mbele yetu,” amesema Kagoma na kuongeza;

“Matarajio ni makubwa na wanatambua wapo kundi gumu lakini wao kama wachezaji wamejiandaa kwenda kupambania nembo ya taifa kwa kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye michuano hiyo.”

Hii ni mara ya nne kwa Tanzania kushiriki fainali hizo baada ya zile za 1980 kule Nigeria, 2019 zilizofanyikia Misri na fainali zilizopita za 2023 Ivory Coast na mara zote haijawahi kutoka na ushindi katika hatua ya makundi achilia mbali kuvuka kwenda hatua inayofuata ya michuano hiyo.

Stars ipo chini ya kocha Miguel Gamondi kabla ya kuanza kwa mashindano hayo tayari imecheza mechi mbili za kirafiki ikianza dhidi ya Haras El Hodoud ikiibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Morice Abraham na mchezo wa pili walicheza na Arab Constracors na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.