WIZARA YA FEDHA :WATAALAM WA UNUNUZI ZINGATIENI DIRA YA MAENDELEO YA 2050

Na Vero Ignatus, Arusha

WIZARA ya Fedha imewataka wataalamu wa Ununuzi na Ugavi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 ili kuimarisha utawala bora.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, kwa niaba ya Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Munde, wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 16 wa Mwaka wa Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) uliofanyika Jijini Arusha

Balozi Omar alisema ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ni muhimu kwa PSPTB kutekeleza shughuli zake kwa kuzingatia dira hiyo.

“Serikali imeelekeza kuwa shughuli zote za ununuzi na ugavi nchini ziunganishwe na mfumo wa NeST ili kuleta uwazi, uwajibikaji na kuhakikisha thamani ya fedha,”

Aliongeza kuwa, “Hata mfumo wa usajili wa wataalamu wa ununuzi na ugavi wa PSPTB umeunganishwa na NeST ili kuhakikisha kunakuwepo wataalamu wenye sifa stahiki.”

Kwa mujibu wake, kwa kuwa asilimia 70 ya bajeti ya serikali inaelekezwa kwenye sekta ya ununuzi na ugavi, ni muhimu kwa waajiri kuruhusu wafanyakazi wao kuhudhuria mikutano ya kila mwaka ya PSPTB ambayo huwasaidia kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia taaluma.

Hata hivyo, Balozi Omar alionya na kukemea wale wanaotekeleza shughuli za ununuzi na ugavi bila kuwa na sifa stahiki, hususan katika serikali za mitaa, akisema kuwa wanakiuka Sheria ya Ununuzi na Ugavi jambo ambalo halikubaliki.

Katika hatua nyingine, aliihimiza sekta binafsi pia kutekeleza shughuli zao za ununuzi na ugavi kwa mujibu wa sheria za nchi katika sekta husika.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa PSPTB, Jacob Kibona, alisema baadhi ya mafanikio ya PSPTB kuwa ni pamoja na kusimamia na kuendeleza mitaala ya kitaaluma kwa lengo la kuzalisha wataalamu wenye uwezo.

Mafanikio mengine aliyoyataja ni kutoa mafunzo endelevu ya maendeleo ya kitaaluma, pamoja na kuboresha matumizi ya mifumo ya kidijitali kama vile mfumo wa usajili.

Kwa mujibu wake, PSPTB imefanikiwa kuwajengea uwezo wataalamu 3,164 wa ununuzi na ugavi.

Akizungumzia changamoto, Kibona alisema PSPTB inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa wakaguzi (auditors) wenye sifa stahiki, hususan katika ngazi ya serikali za mitaa, pamoja na baadhi ya halmashauri kutumia wakaguzi wasiokuwa wa taaluma ya ukaguzi, hali inayosababisha upotevu wa fedha za umma na kutolewa kwa taarifa duni za ukaguzi.

Wakati huo huo, Wakati huo huo, Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Biashara kutoka Kampuni ya Magazeti ya Serikali(TSN) , Soter Salema alisema kampuni hiyo inajivunia safari ya mageuzi ya teknolojia kupitia Tehama ikiwemo utunzaji wa kumbukumbu za picha na historia mbalimbali za kuandika “Archivers”

Alisema TSN inajivunia kuhifadhi nyaraka ikiwemo kuzipanga na kuhifadhi kwa usalama na kuhakikisha taarifa zinapatikana kwa matumizi ya baadaye ikiwemo kulinda kumbukumbu za kihistoria, kisheria au kitaasisi

“TSN tunahakikisha tunatumia Tehama katika kuhakikisha nyaraka za serikali zinahifadhiwa kwa usalama sanjari na utunzaji wa vitabu vyenye historia mbalimbali”