Baresi akitua tu, Lamela atafuata KMC

UONGOZI wa KMC unaendelea na mchakato wa kusaka kocha mpya atakayerithi nafasi ya Mbrazil Marcio Maximo, huku mabosi wa kikosi hicho wanaangalia uwezekano wa kuipata saini ya kiungo mshambuliaji wa KVZ ya Zanzibar, Yusuph Mfaume ‘Lamela’.

Kiungo huyo inaelezwa atakamilisha uhamisho huo wa kujiunga na kikosi hicho, ikiwa Abdallah Mohamed ‘Baresi’ anayetajwa kurithi mikoba ya Maximo atakamilisha dili la kutua ndani ya timu hiyo kutokana na uhusiano mzuri kati ya pande mbili.

Maximo aliachana na kikosi hicho Desemba 6 akidumu kwa siku 131, tangu alipotambulishwa Julai 28 mwaka huu akiiongoza katika Ligi Kuu kucheza mechi tisa na kushinda moja, sare moja na kupoteza saba, huku timu hiyo ikifunga mabao mawili tu na kufungwa 14.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza Lamela ni mapendekezo ya kocha Baresi anayeifundisha kwa sasa Zimamoto ya Zanzibar, ambapo ameonyesha nia ya kujiunga na KMC, ikiwa mazungumzo waliyokubaliana mwanzoni yatatimia.

“Katika mazungumzo yetu na Baresi alimtaja Lamela lakini kwa bahati mbaya sisi hatujawahi kumfuatilia, suala la yeye kukubaliana kuja tusubirie kwanza, ingawa kuanzia Jumatatu tutakuwa tuko sehemu nzuri zaidi,” amesema kigogo wa KMC.

Kiongozi huyo amesema mchezaji kupendekezwa na kocha ni jambo nzuri kwa sababu ndiye anayemjua zaidi na jinsi ambavyo atamtumia, ingawa kwa sasa ni mapema kuzungumzia usajili huo, hadi pale watakapokamilisha taratibu za benchi la ufundi.

Baresi mara ya mwisho kufundisha timu ya Ligi Kuu Bara, ilikuwa ni maafande wa Mashujaa, ambayo aliachana nayo Februari 26, 2025.