Dk Mwigulu ataka TRA kuweka mabango  miradi iliyotekelezwa kwa kodi za wananchi

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameilekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuweka mabango kwenye miradi iliyotekelezwa kwa kodi za wananchi, ili kuonyesha namna Watanzania waliyoshiriki kuijenga.

Mtendaji huyo mkuu wa shughuli za Serikali, amesema hatua hiyo itawezesha Watanzania kutambua namna ambavyo fedha zao zinavyotumika kupitia kodi wanazozilipa.

Dk Mwigulu ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Desemba 20, 2025 wakati akikagua ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Lindi, katika mwendelezo wa ziara yake ya kikazi iliyoingia siku ya pili mkoani humo.

Amefafanua kuwa kumekuwa na utaratibu Serikali ikipokea hata msaada wa choo, basi bango la tangazo litawekwa likionyesha ujenzi wa mradi umetekelezwa kwa hisani ya watu wao, lakini iliyotekelezwa kwa fedha za ndani haiwekewi alama.

“Sasa niwaelekeze TRA, inapofanyika miradi mikubwa kama huu na umejengwa kwa fedha za Watanzania au mradi mkubwa kama ule wa bandari uliogharimu Sh280 bilioni. Pia mradi wa Bwawa la umeme la Nyerere (Sh6 trilioni), waweke bango kuonyesha imejengwa kwa fedha za Watanzania.

“Waipitie miradi yote iliyokamilika na inayoendelea kujengwa kuhakikisha kabla ya siku ya uzinduzi na siku ya uzinduzi watu walione hilo bango kwamba Watanzania wenyewe wamejenga mradi huu,” ameeleza.

Dk Mwigulu amesema Watanzania wametoa mchango mkubwa katika maendeleo, ikiwemo ununuzi wa mashine za CT-Scan, MRI katika hospitali mbalimbali za mikoa kupitia kodi zao.

Katika ziara hiyo, Dk Mwigulu amesema kumekuwa na kilio cha dawa muhimu kukosekana katika maeneo mengi, licha ya kuwepo kwa majengo mazuri ya vituo vya afya, zahanati na hospitali zenye vipimo vya kisasa.

“Inajitokeza mgonjwa anaonana na daktari na kuhudumiwa vizuri, lakini inaonekana dawa mahsusi anayotakiwa kutibiwa haipo hospitalini. Hili limekuwa likileta dosari, na wagonjwa wanaelekezwa wakatafute dawa nje,”

“Sasa hospitali kubwa kama hii, inatakiwa kuwa na duka la dawa zote  muhimu, Naibu Waziri wa Afya (Dk Florence Samizi), fuatilieni vizuri kitengo cha utafiti wa dawa na Bohari ya Dawa (MSD) inayoagiza dawa,” amesema.

Dk Mwigulu ametahadharisha kuwa isiwe kukawa kunafanyika ujanja katika baadhi ya maeneo, akisema haiwezekani hospitali kubwa zikiwemo za mikoa zikose dawa, lakini kwenye maduka binafsi zipo.

“Ukienda hospitali kila mgonjwa anaelekezwa hii dawa haipo hapa akatafute sehemu nyingine, hili halikubaliki. Kwa kuwa tunaelekea kwenye bima ya afya kwa wote, basi tunaamini itampa vyote akiwa hospitalini,” amesema Mwigulu.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Alexander Makalla amesema ujenzi wa hospitali hiyo ulianza mwaka 2021 na hadi kukamilika kwake utagharimu Sh30.9 bilioni.

Dk Makalla amesema hospitali hiyo ya rufaa, itakuwa na majengo manne yakiwemo ya huduma za msingi,  huduma za wagonjwa wa nje, CT-Scan, mionzi, wagonjwa wa dharura na wagonjwa mahututi (ICU) na tayari huduma zimeanza kutolewa.

Kwa upande wake, Dk Samizi amesema hospitali hiyo ya rufaa itakuwa na uwezo wa kuona wagonjwa 150 hadi 200 kwa siku, lakini wanaojifungua watakuwa zaidi ya saba kutoka watatu, kutokana na maboresho yanayoendelea kufanyika.