FCT YAIMARISHA ELIMU YA USHINDANI KWA WADAU MBEYA

BARAZA la Ushindani (FCT) jana Desemba 18, 2025, limeendesha semina ya elimu kwa wadau mkoani Mbeya kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu majukumu na huduma zinazotolewa na Baraza hilo.

Semina hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na kufunguliwa na Katibu Tawala Msaidizi – Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mkoa wa Mbeya, Bi Anna Mwambene, ambaye aliwahimiza wadau kutumia ipasavyo mifumo ya kisheria iliyopo na kuwa mabalozi wa kuitangaza huduma za Baraza la Ushindani.

Bi Mwambene alisema uelewa wa sheria na taratibu za ushindani ni muhimu katika kukuza mazingira bora ya biashara na uwekezaji, akisisitiza umuhimu wa wadau kushiriki kikamilifu katika kulinda haki zao kwa kutumia mifumo rasmi iliyowekwa na Serikali.

Katika semina hiyo, Baraza la Ushindani liliwapatia washiriki elimu kuhusu matumizi ya mfumo wa kidijitali wa kuwasilisha rufaa zinazotokana na maamuzi ya Tume ya Ushindani (FCC) pamoja na mamlaka mbalimbali za udhibiti, zikiwemo LATRA, EWURA, TCRA, TCAA na PURA.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa TEAMA wa Baraza la Ushindani, Bw Athuman Kanyegezi, alisema mfumo huo unamwezesha mtumiaji kuanzisha akaunti, kuwasilisha rufaa kwa njia ya mtandao, kupakia nyaraka husika, kulipa ada na kufuatilia hatua za mwenendo wa kesi bila kulazimika kufika ofisini.

Aliongeza kuwa matumizi ya mfumo wa kidijitali yanalenga kurahisisha upatikanaji wa haki, kuongeza uwazi na kupunguza gharama na muda kwa wadau wanaohitaji huduma za Baraza hilo.

Semina hiyo iliwahusisha wafanyabiashara, wajasiriamali na wawakilishi wa taasisi mbalimbali, ambapo washiriki walipata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi kuhusu taratibu za rufaa na utoaji wa haki kwa njia ya kidijitali.