Dar es Salaam. Katika wakati ambao amani na umoja wa kitaifa vinakabiliwa na changamoto za kisiasa na kijamii, fikra za Mwalimu Julius Nyerere, zimetajwa kuwa dira muhimu ya kulinda mshikamano na umoja wa Watanzania.
Hoja hiyo imeibuliwa na wajumbe wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere wakati wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa taasisi hiyo, uliofanyika leo Jumamosi, Desemba 20, 2025, jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, wajumbe wameeleza kuwa urithi wa fikra na falsafa za Mwalimu Nyerere unaendelea kuwa dira muhimu katika kulinda amani, kuimarisha umoja wa kitaifa na kuongoza mwelekeo wa demokrasia nchini.
Akizungumza kuhusu msingi wa falsafa ya Mwalimu katika kudumisha amani na umoja, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa taasisi hiyo na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, amesema Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi wa kipekee aliyesimamia kwa dhati maadili, uadilifu na mshikamano wa kitaifa, huku akipinga vikali rushwa, ubinafsi na uzembe katika uongozi.
“Mwalimu akikuwa mkali sana kwa rushwa, alikuwa hapendi kabisa mbwembwe, serikalini” amesema Pinda, akiongeza kuwa uongozi wa aina hiyo ndio ulioweka misingi imara ya amani na utulivu wa Taifa.
Pinda amefafanua kuwa amani ilikuwa nguzo kuu ya fikra za Mwalimu, akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila amani na umoja katika jamii.
“Mwalimu alisimamia sana kitu kinachoitwa amani, alisisitiza kuwa ukiondoa amani hakuna maendeleo,” amesema.
Akirejea matukio yaliyotokea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Waziri Mkuu huyo wa zamani amesema kujifungia ndani kwa siku sita pekee kulikotokana na vurugu za uchaguzi, kulithibitisha fikra za Mwalimu kuwa amani ikikosekana hakuna maendeleo.
Akitaja njia alizotumia Mwalimu kujenga amani, Pinda amesema kwa mtazamo wa Mwalimu, amani hujengwa na watu kupitia umoja na mshikamano wa kitaifa na kwamba pasipo na umoja amani nayo hutoweka.
Kiongozi huyo mkongwe nchini amerejea historia ya Taifa, akibainisha kuwa uhuru wa Tanganyika na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar vilipatikana bila kuvuruga amani, akisisitiza kuwa madai ya mabadiliko hayapaswi kuhusisha uvurugaji wa amani na umoja nchini.
“Hauwezi kutaja uhuru bila kumtaja Mwalimu, vivyo hivyo hauwezi kuutaja Muungano bila kuwataja Mwalimu na Karume, yote hayo yalifanyika bila kuathiri amani na umoja,” amesema.
Katika muktadha wa demokrasia, Pinda amekumbushia historia ndefu ya safari ya demokrasia akieleza kuwa licha ya wananchi wengi kutaka mfumo wa chama kimoja, mwelekeo wa dunia ulihitaji mabadiliko.
“Kama Taifa lazima tuzungumze tupo wapi na tunaelekea wapi, watu wajue fikra za Mwalimu na historia ya demokrasia yetu.
“Katika mchakato wa demokrasia licha ya walio wengi wakati huo kutaka mfumo wa chama kimoja, kwa kuangalia mwelekeo wa dunia Tume ya Nyalali (Jaji Francis) ilishauri tuende kwenye vyama vingi, cha kushangaza, Mwalimu mwenyewe aliamua twende huko,” amesema akitafsiri uamuzi huo kama mfano wa uongozi unaotanguliza maslahi amani na umoja wa Taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Paul Kimiti, amesema taasisi hiyo imekuwa chombo muhimu cha kuenzi na kutangaza fikra za Mwalimu ndani na nje ya nchi.
Kimiti amebainisha kuwa mvuto wa taasisi hiyo umeanza kuvuka mipaka ya Tanzania na kuwashawishi wanasiasa kutoka mataifa jirani waliomfahamu Mwalimu kutaka kujiunga nayo.
“Hivi karibuni Rais wa Uganda, Yoweri Museveni alisema amekuwa akiisikia taasisi hii naye anavutiwa kuwa sehemu ya wajumbe,” amesema Kimiti, akionyesha namna urithi wa Mwalimu unavyoendelea kuheshimiwa kimataifa.
Kimiti pia ameeleza kuwa katika nyakati za taharuki zinazotishia amani na umoja wa kitaifa, jamii inapaswa kutafakari kwa kina fikra za Mwalimu katika kulinda amani ili kuepuka kuvuruga misingi aliyoiasisi.
“Siku ya Oktoba 29, 2026 nilipoona yaliyotokea nilikaa chini kumuomba Mwalimu Nyerere huko aliko nchi yetu ibaki katika amani, Baba wa Taifa hakutuachia maandamano, alituachia amani,” amesisitiza.
Mwanzilishi wa wazo la kuanzishwa kwa taasisi hiyo, Mtiti Mbasa, amesema dhamira ya kuanzishwa kwa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, ni kuenzi fikra za Mwalimu kama urithi wa Taifa katika kudumisha amani na umoja wa Kitaifa.
“Nilianzisha wazo hili kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa fikra zake katika kuhakikisha amani na umoja wa kitaifa unadumishwa,” amesema.
Ameafanua kuwa ili kufikia lengo hilo, taasisi hiyo inajipanga kuifikia jamii moja kwa moja kupitia uwakilishi katika ngazi mbalimbali za kijamii.
“Ili jamii imuenzi vyema Mwalimu, tunahitaji kurejesha misingi ya kijamii aliyoiimarisha, hususan elimu na uzalendo, natamani zile nyimbo za kizalendo tulikuwa tunaimba shuleni enzi zile zingerudi tena,” amesema mjumbe mwingine, Juma Mninga.
Akitaja mbinu zingine zinazochukuliwa na taasisi hiyo, Chifu Japhet Wanzagi, mlinzi wa familia ya Baba wa Taifa huko Butiama, amesema jamii inapaswa kufundishwa kumuenzi Mwalimu kwa vitendo.
“Niliishi na Mwalimu enzi za uhai wake, alikuwa mtu aliyeipenda sana nchi yake, Mwalimu alifundisha kwa vitendo, akifanya kazi kwa mikono yake na kuwajengea vijana maadili ya kazi na uzalendo,” amesema.
