Ibenge ataka wawili tu Azam FC

KIKOSI cha Azam FC kipo mapumziko kwa sasa baada ya Ligi Kuu Bara kusimama kupisha fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zitakazoanza kesho huko Morocco, lakini benchi la ufundi la timu hiyo halijalala kutokana na kuanza msako wa nyota wawili wapya.

Azam kwa sasa ipo nafasi ya tisa kwa kukusanya pointi tisa kupitia mechi tano, huku ikicheza makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa kundi B bila pointi baada ya mechi mbili za awali, hatua iliyomfanya kocha Florent Ibenge kutaka kuimarisha kikosi kupitia dirisha dogo.

Kocha huyo wa zamani wa AS Vita ya DR Congo, RS Berkane ya Morocco na Al Hilal ya Sudan ameuambia uongoza wa klabu hiyo kuwa anahitaji majembe mawili tu ya maana katika dirisha dogo, mmoja akiwa ni beki na mwingine kiungo mshambuliaji ili kila kitu kikae sawa klabuni.

IBE 01

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, zinasema Ibenge amewasilisha ripoti kwa uongozi ikieleza maeneo mawili yanayohitaji maboresho ya haraka ambayo ni ulinzi wa kati na kiungo mshambuliaji, kutokana na kuwepo kwa hofu ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye anatajwa kuwa mbioni kuondoka.

“Kwa upande wa ulinzi, Ibenge ameonyesha haja ya kuongeza beki mwenye uzoefu na uwezo wa kuongoza safu ya nyuma. Licha ya Azam kuwa na mabeki wenye vipaji, kumekuwa na makosa madogo yanayogharimu timu katika mechi nyingi hasa wanapokutana na timu zinazocheza kwa kasi na mipira ya juu,” chanzo hicho kilisema.

Chanzo hicho kimeongeza hadi sasa Azam  haina uhakika sana kama Fei ataendelea kusalia kutokana na ofa nzito zinazoendelea kupokewa, japo mkataba na kiungo huyo ukiwa bado haujamalizika, jambo linalodaiwa limemfanya hata Ibenge kuanza mapema kusaka kiungo mshambuliaji mwingine.

“Ingawa wachezaji waliopo wamekuwa wakijitahidi, bado benchi la ufundi linaamini hakuna aliyefikia kiwango cha kuamua mechi kwa ubunifu, pasi za mwisho na mabao muhimu kama anavyofanya Fei.

“Ni kama maandalizi yameanza mapema ili kama ikitokea Fei ameuzwa basi kuwe na mrithi ambaye ana kiwango bora kama yeye au zaidi yake na huenda akawa wa kigeni,” kilifafanua chanzo hicho na kuongeza;

“Siwezi kusema ataondoka dirisha dogo ila msimu ujao ni ngumu kuweka uhakika wa kuwa naye hivyo Ibenge na viongozi ni kama wameanza kujipanga mapema.”

IBE 02

Mwanaspoti linafahamu kuwa, uongozi wa Azam umeipokea ripoti hiyo, huku vikao vya ndani vikiendelea kujadili majina ya wachezaji wa ndani na nje ya nchi wanaoweza kuingia katika mipango hiyo.

Mabeki wa kati Azam kwa sasa ni pamoja na Yeison Fuentes, Edward Manyama, Lameck Lawi, Yoro Diaby na Ahoutou Zouzou, wakati kwa kiungo mshambuliaji mbali na Fei, kuna majembe mengine yakiwamo wazawa na wageni, ila Ibenge ametaka kuletewa mtu wa kazi kuboresha eneo hilo.

Mara michuano ya CAF itakaporejea, Azam itakuwa na kibarua mbele ya Nairobi United ambayo kama wao haina pointi na kila moja imepoteza mechi mbili na kuruhusu mabao matatu, na pia itakuwa na kibarua cha mechi za Ligi Kuu na kwa sasa inaelezwa ipo mbioni kushiriki Kombe la Mapinduzi 2026.