Kocha Mashujaa awapa kazi mastraika

KOCHA Mkuu wa Mashujaa Queens, Ally Ally amesema kikosi chake kimefikia asilimia 80 ya ubora anaoutaka msimu huu kwenye Ligi Kuu ya Wanawake, huku akijipa mechi tano kukamilisha asilimia 20 zilizobaki.

Mashujaa Queens ya Kigoma inakamata nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo baada ya kuvuna alama sita katika mechi tatu na imeshinda mbili na kupoteza moja, huku ikifunga mabao saba na kuruhusu mawili.

Timu hiyo iko nyuma ya vinara wanaochuana katika nafasi ya kwanza, JKT Queens, Simba Queens na Yanga Princess zenye alama tisa kila moja, huku zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Kocha Ally aliyeipa ubingwa wa ligi hiyo JKT Queens msimu wa 2016-2017 na 2017-2018, alisema wachezaji wa kikosi hicho wanakwenda vizuri mpaka sasa japokuwa kuna makosa machache hususan eneo la ushambuliaji ambalo wanaendelea kulishughulikia.

“Mpaka sasa naridhishwa kwa asilimia 80 na mwelekeo tunaokwenda nao, tupo vizuri, ni makosa madogo hasa safu ya ushambuliaji ndio tunazidi kuiboresha uwanja wa mazoezi,” alisema Ally.

Alisema hawatakurupuka kufanya usajili dirisha dogo kwa sababu wanataka kujiridhisha na wachezaji waliopo, hivyo amejipa walau mechi tano za ligi hiyo ili kufanya uamuzi wapi aboreshe.

“Kuhusu mipango ya dirisha dogo mpaka sasa bado sijajua, ngoja tucheze mechi kama tano hivi niangalie kwanza timu inakwendaje,” alisema kocha huyo.