Mwigulu aagiza dawa mahsusi kupatikana hospitalini

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameutaka uongozi wa Wizara ya Afya ufuatilie suala la upatikanaji wa dawa mahsusi hospitalini, ili kuondoa dosari ndogondogo zilizopo.

Ametoa maagizo hayo leo Jumamosi, Desemba 20, 2025 wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Lindi na viongozi wa sekta ya afya, mara baada ya kupokea taarifa ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi inayojengwa katika eneo la Mitwero, nje kidogo ya mji wa Lindi.

“Kitengo chenu cha utafiti kifanye kazi kubaini ni aina gani ya dawa zinahitajika hapa mkoani Lindi. Bohari ya Dawa ifuatilie vizuri na kuleta dawa zinazotakiwa,” amesema akimwagiza Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi ambaye alikuwepo katika ziara hiyo.

Muonekano wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi.

Amesema usipofanyika utafiti huo, Bohari ya Dawa watajikuta wanapeleka dawa nyingi mahali ambako hazihitajiki.

“Unaweza kujikuta unapeleka dawa nyingi za malaria huko Zanzibar wakati wao hilo tatizo hawana kabisa.Kuna kilio cha dawa mahsusi kukosekana katika hospitali na badala yake wagonjwa wanaambiwa waende kununua kwenye vioskI. Takwimu zinaonyesha kuna utoshelevu wa dawa wa asilimia 80 – 90 lakini katika hali halisi, watu wanaambiwa wakanunue dawa nje,” ameeleza.

Kuhusu upatikanaji wa vifaa tiba, Waziri Mkuu amesema ndani ya miaka minne na nusu, Rais Dk Samia Suluhu Hassan ameweza kuweka mashine za CT-Scan katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara ikilinganishwa na mashine mbili zilizokuwepo.

“Pia ameweka mashine za MRI katika hospitali zote za kanda ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibingwa,” amesema.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba leo Desemba 20,2025 akikagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, pamoja na kusalimia baadhi ya wananchi wanaopata huduma katika hospitali hiyo

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Alexander Makalla amesema ujenzi wa hospitali hiyo ulianza mwaka 2021 na hadi kukamilika kwake utagharimu Sh30.9 bilioni.

Dk Makalla amesema hospitali hiyo ya rufaa, itakuwa na majengo manne yakiwemo ya huduma za msingi,  huduma za wagonjwa wa nje, CT-Scan, mionzi, wagonjwa wa dharura na wagonjwa mahututi (ICU) na tayari huduma zimeanza kutolewa.

Kwa upande wake, Dk Samizi amesema hospitali hiyo ya rufaa itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 150 hadi 200 kwa siku, lakini wanaojifungua watakuwa zaidi ya saba kutoka watatu, kutokana na maboresho yanayoendelea kufanyika.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amekagua maendeleo ya mradi wa shule mpya ya msingi ya Likong’o inayojengwa kwa ushirikiano baina ya mradi wa gesi asilia (LNG) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Shule hiyo iliyopo katika kijiji cha Likong’o itakapokamilika, itagharimu Sh1.2 bilioni ambapo kati ya fedha hizo, Serikali imechangia asilimia 26.68, kampuni ya Shell imechangia asilimia 36.66 na kampuni ya Equinor imechangia asilimia 36.66.