SINGIDA Black Stars imeelekeza nguvu zake kwa beki wa kimataifa wa DR Congo, Henock Inonga, kama chaguo la kwanza kwa ajili ya kuimarisha ukuta wa kikosi hicho dirisha dogo la usajili linalotarajiwa kufunguliwa Januari Mosi 2026 kutokana na mapendekezo ya Kocha Miguel Gamondi.
Taarifa kutoka katika klabu hiyo, zinaeleza Gamondi amekuwa akihitaji beki wa kati mwenye uzoefu mkubwa na uwezo wa kuhimili presha ya mechi kubwa, jambo linalomfanya Inonga kuibuka kama jina linalopewa uzito zaidi kuliko machaguo mengine yaliyopo.
Inonga, ambaye kwa sasa hana timu baada ya kumaliza mkataba wake na FAR Rabat ya Morocco, inaelezwa yupo tayari kurejea Ligi Kuu Bara, hatua inayoipa Singida fursa ya kumsajili.
Uamuzi wa Singida kumtazama Inonga kwa karibu umechochewa pia na changamoto za kiufundi zinazoikabili timu hiyo na Gamondi amelazimika kumrudisha kiungo Morice Chukwu kucheza nafasi ya beki wa kati akishirikiana na Antony Tra Bi, hali inayoonesha wazi kocha huyo bado hajaridhishwa na kiwango cha mabeki wa asili waliopo kikosini.
Licha ya kuwa na mabeki wengine kama Mukrim Issa na Kennedy Juma, matumizi ya Chukwu katika safu ya nyuma yameibua maswali juu ya uimara wa ukuta wa Singida, huku Gamondi akitafuta beki mwingine.
Kwa upande wake, Inonga ana rekodi ya kucheza katika mazingira ya ushindani mkubwa barani Afrika, ikumbukwe kuwa beki huyo aliwahi kutamba nchini akiwa na Simba, hivyo uzoefu wake unaoonekana kumvutia Gamondi ambaye anaamini beki huyo anaweza kuongeza kitu katika kikosi hicho kinachoshiriki pia Kombe la Shirikisho Afrika kikiwa hatua ya makundi.
Iwapo mazungumzo yatafanikiwa, Inonga anatarajiwa kuwa suluhisho la Singida Black Stars katika harakati zao za kuimarisha kikosi kuelekea nusu ya pili ya msimu.