Dar/Mwanza. Je, taka za plastiki zinasababisha saratani? Ni swali linalogonga vichwa, huku wataalamu wakifanya utafiti kubaini namna chembechembe za plastiki ‘microplastiki’ zinavyoingia kwenye mwili wa binadamu kwa njia tofauti, ikiwamo vyakula.
Hatari ipo kwenye maeneo ya mito, bahari na maziwa ambako taka za plastiki hutupwa ovyo.
Hata hivyo, hakuna ushahidi wa moja kwa moja na wa mwisho unaothibitisha kuwa microplastiki pekee husababisha saratani kwa binadamu, lakini kazi za kitafiti za kisayansi zinaonesha kuna hatari inayoweza kujitokeza, hasa kwa njia zisizo za moja kwa moja.
Microplastiki ni chembe ndogo sana za plastiki (chini ya milimita tano) zinazopatikana kwenye maji ya kunywa, chakula (samaki, chumvi, sukari), hewa tunayovuta na vifaa vya plastiki.
Huhusishwa na hatari ya saratani kutokana na kuchochea msongo wa oksidizesheni (oxidative stress) kwenye seli, hali inayoweza kuharibu vinasaba (DNA), ambavyo ni moja ya nguzo kuu za kuibuka kwa saratani.
Pia, husababisha uvimbe wa muda mrefu kwa kuwa chembe hizi za plastiki zikikaa mwilini kwa muda mrefu, zinaweza kuchochea mwitikio wa kinga unaoleta uvimbe sugu ambao huongeza hatari ya saratani.
Vilevile, hubeba kemikali hatarishi (kama BPA, phthalates) na sumu kutoka kwenye mazingira (metali nzito, viuatilifu).
Baadhi ya kemikali hizi huathiri mfumo wa homoni, ambazo zikivurugika zinaweza kuongeza hatari ya saratani kama ya matiti au tezi dume.
Kazi za kitafiti zimefanyika kwa wanyama au maabara, si kwa binadamu moja kwa moja ambazo zimegundua uwepo wa chembe hizo kwenye mapafu, damu, kondo la nyuma na kinyesi cha binadamu, jambo linaloonesha microplastiki huingia mwilini.
Miongoni mwa kazi hizo hizo ni utafiti uliohusisha jarida la utafiti kuhusu maziwa makuu, uliobaini kemikali za BPA na ‘phthalates’ zinazotambulika kimaabara kwa kuvuruga homoni, hivyo kuongeza hatari ya saratani.
Utafiti umefanywa na Fares Biginagwa na wenzake wenye jina: “Ushahidi wa kwanza wa microplastiki katika Maziwa Makuu Afrika: Ugunduzi kwenye sato na sangara wa Ziwa Victoria” mwaka 2015 na kuchapishwa na jarida la mtandaoni la ScienceDirect.
Utafiti huo ulifanyika Mkoa wa Mwanza, Tanzania, ulio pwani ya kusini ya Ziwa Victoria.
Utumbo wa samaki waliovuliwa kienyeji aina ya sangara na sato ulichunguzwa kubaini uwepo wa microplastiki, ambazo zilithibitishwa katika asilimia 20 ya jamii hizo za samaki kwa kutumia mbinu ya kitaalamu, vyanzo ikielezwa inaweza kuwa taka zinazotupwa majini.
“Ingawa tafiti zaidi zinahitajika ili kutathmini kikamilifu athari za uchafuzi wa plastiki katika eneo hili, utafiti wetu ni wa kwanza kuripoti uwepo wa plastiki kwa jamii ya samaki katika Maziwa Makuu ya Afrika,” inaeleza sehemu ya utafiti huo.
Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk Crispin Kahesa, anasema hadi sasa hajaona utafiti wowote unaoonyesha uhusiano kati ya saratani na taka za plastiki. Hata hivyo, anasema kuna haja ya tafiti zaidi kufanyika katika eneo hilo kubainisha hatari iliyopo.
Anasema saratani inayoongoza kwa sasa nchini Tanzania ni ya shingo ya kizazi ambayo inasababishwa na virusi vya HPV, ikifuatiwa na tezi dume na saratani ya njia ya chakula. Anasema hizo zote hazisababishwi na plastiki.
“Katika orodha ya saratani 10 zinazoongoza Tanzania, hakuna hata moja ambayo inahusishwa na plastiki, kwa hiyo hayo madai yako kinadharia zaidi,” anasema.
Mwananchi lilitembelea eneo la Ziwa Victoria kwa upande wa Mwanza na Bukoba, mkoani Kagera na kubaini uwepo wa taka za plastiki kando mwa ziwa, jambo linalohatarisha siyo tu uhai wa viumbe maji, bali pia afya za binadamu.
Taka za plastiki kama chupa za vinywaji na mabaki ya nyavu, zimeonekana katika mwambao wa ziwa hilo katika baadhi ya maeneo, jambo linaloibua maswali kuhusu uwajibikaji wa mamlaka katika udhibiti wa taka hizo.
David Mgeta, mvuvi katika Kisiwa cha Bezi, wilayani Ilemela, mkoani Mwanza, anasema wamekuwa wakipewa elimu na mashirika ya uhifadhi wa mazingira kwa kushirikiana na Serikali kuhusu uchafuzi wa ziwa unavyoweza kuathiri uvuvi na afya za watumiaji wa samaki.
“Tumejipangia utaratibu, kila Jumamosi ni siku ya usafi. Tuna maeneo maalumu ya kuhifadhi taka. Uongozi wetu unafuatilia, mvuvi atakayebainika kuacha nyavu ziwani ama kutupa chupa au uchafu wowote anachukuliwa hatua,” anasema na kuongeza:
“Hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kutozwa faini au kufukuzwa huku (kisiwani) kwa sababu sisi wavuvi asilimia kubwa siyo wakazi wa huku, ni watafutaji tu kulingana na upatikanaji wa samaki.”
Katika mwalo wa Nyamkazi, ulioko Bukoba, Almachius Deus, anasema amekuwa akishuhudia uwepo wa taka za plastiki ziwani, lakini hajui madhara yanayoweza kusababishwa na uwepo wake.
“Nashauri Serikali itoe elimu zaidi kwa watumiaji wa samaki na wavuvi kwa ujumla kuhusu madhara ya taka za plastiki ili tutunze mazingira. Pia, tupunguze athari kwa afya zetu hasa kwa sisi walaji wa samaki,” anasema.
Mvuvi mwingine katika mwalo huo, Godfrey Anatory, anasema baada ya taka kuzidi ziwani, Serikali iliweka mtu maalumu wa kuziokota, huku wananchi katika eneo hilo wakichangisha fedha ili kufanikisha kazi hiyo.
“Nashauri wazidi kuongeza juhudi, waokota uchafu wawe wengi ili tukae katika mazingira safi,” anasema mvuvi huyo ambaye pia ni mchuuzi wa samaki na dagaa mwaloni hapo.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU), Hashim Rashid, anasema wao kama viongozi wa mwalo wa Nyamkazi hawaruhusu chupa za plastiki kuonekana katika eneo hilo.
Lakini anasema kuna mito inayopeleka maji ziwani, hivyo mvua zinaponyesha taka mbalimbali huingia ziwani zikiwamo za plastiki.
Anasema Serikali imepiga marufuku nyavu za plastiki zikiwamo ‘malumalu’ ambazo amesema haziozi, jambo linalohatarisha usalama.
“Kuna Mto Kanoni, kuna Mto Kenumi ukienda maeneo hayo utakuta chupa nyingi ambazo hazitoki hapo, zinatoka sehemu nyingine, hiyo ni changamoto. Hatujawahi kuona samaki amekula chupa za plastiki lakini tunasikia wataalamu wanatuwambia hivyo,” anasema.
Kutokana na umuhimu wa usafi, anasema wapo watu wanalipwa kwa ajili ya kuondoa uchafu mwaloni na hasa chupa za plastiki.
Vitus Audax, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Synergistic Globe linalojihusisha na utunzaji na uhifadhi wa mazingira anasema:
“Hali ya usimamizi wa taka za plastiki katika Ziwa Victoria bado ipo chini kutokana na kukithiri kwa taka hizo, hususani maeneo ya mialo yanayokusanya jumuiya ya watu wengi wenye hulka tofauti.”
Anasema mwaka 2015, utafiti uliofanywa kupitia sampuli za samaki aina ya sangara na sato waliotolewa ndani ya Ziwa Victoria mkoani Mwanza, ulibaini asilimia 20 ya samaki hao walikuwa na chembe za plastiki, sawa na kusema kati ya samaki watano ndani ya ziwa hilo, mmoja ana chembe za plastiki.
“Hii ni hatari kwa jamii yetu na wote wanaozunguka mikoa ya Kanda ya Ziwa kwani mara kadhaa tunaambiwa na wataalamu wa afya kuwa maradhi ya saratani yamekithiri kwenye mikoa hii huku hali hiyo ikihusishwa pia na vyakula ikiwemo samaki,” anasema.
Hata hivyo, Dk Kahesa kutoka ORCI anasema taarifa hizo si sahihi kwa sababu wao wanapokea wagonjwa wengi kutoka kanda ya mashariki, yaani mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Anasema hilo limechangiwa zaidi na wingi wa idadi ya watu katika eneo hilo, pamoja na urahisi wa kufikika kwa ajili ya huduma hizo kwani wagonjwa kutoka mikoa ya jirani huamua kwenda Ocean Road kupata matibabu.
“Mikoa inayozunguka Kanda ya Ziwa ipo mingi, kuna Mwanza, Mara, Geita, Kagera. Kwa hiyo ukiangalia idadi ya watu ya kule, unaweza kuona kuna wagonjwa wengi kwa sababu ya namba, lakini lazima uliweke na ulinganifu kati ya watu 100, wangapi wana saratani,” anasema.
Audax anasema awali walipoanza kutekeleza mradi wa ‘Friends of Lake Victoria’ walibaini taka nyingi za plastiki zikiwamo chupa za maji, juisi na vileo ndizo zimesambaa ziwani.
Amesema wanaendelea kuelimisha jamii kuhusu ulinzi wa ziwa hilo linalotegemewa na watu zaidi ya 40,000 kwa shughuli za uvuvi mkoani Mwanza.
Anaeleza watu zaidi ya milioni 40 wanalitegemea ziwa hilo kwa matumizi tofauti katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, nchi za Afrika Mashariki zinazopitiwa na ziwa hilo pamoja na Misri kupitia Mto Nile unaopokea maji yake kutoka Ziwa Victoria.
Ndalahwa Mabula, Katibu wa Umoja wa Wavuvi wa Magu, Busega na Bunda, anasema hakuna njia rasmi ya kusimamia taka za plastiki, lakini kinachowasaidia ni kwamba zinaweza kurejelezwa, hivyo watu wanaziokota.
