UTT Amis kuangazia soko la Afrika Mashariki na Kusini

Dar es Salaam. Mfuko wa uwekezaji UTT Amis umejipanga kutanua wigo kwa kuangalia fursa zilizopo katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EA) na Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) ili kuwawezesha wananchi wa jumuiya hizo kuwekeza.

Soko hilo linaangaliwa wakati ambao mfuko umerekodi ukuaji wa zaidi ya Sh1.1 trilioni mwaka huu, ukuaji ambao haujawahi kushuhudiwa tangu kuanzishwa kwake.

Hayo yamesemwa jana Desemba 19, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa UTT Amis, Simon Migangala wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano mkuu wa mwaka wa wawekezaji katika mifuko hiyo.

Simon amesema soko la Afrika ya Mashariki na SADC litafikiwa kupitia bidhaa mpya itakayoanzishwa ili kukidhi mahitaji yao.

“Kwa sasa tumeanza kuangalia soko la Afrika ya Mashariki, kadri muda unavyoenda masoko yanaungana na baadaye tutaangalia SADC na siku zijazo tutaanzisha bidhaa ambazo zitagusa soko hili  waliopo nje wenye nia ya kuwekeza Tanzania,” amesema.

Akizungumzia ukuaji ulioshuhudiwa amesema unatokana na mazingira mazuri ya biashara yaliyowekwa hali inayofanya soko la mitaji na fedha likue.

Amesema hilo limefanya ukuaji wa mfuko kuongezeka kutoka Sh2.2 trilioni mwanzoni mwa mwaka hadi mwaka unafungwa ukuaji ukiwa umefikia Sh3.2 trilioni.

Ukuaji wa jumla unashuhudiwa wakati ambao mifuko saba iliyo ndani ya UTT Amis imerekodi faida ya wastani wa asilimia 12.

“Tangu taasisi ianzishwe hatujawahi kufikia ukuaji wa aina hii na hii imechochewa na ukuaji wa uwekezaji na mwanzoni mwa mwaka tulikuwa na watu takribani 300,000 na sasa wako takribani 500,000,” amesema.

Amesema kwa sasa wanatumia teknolojia ili kufanya uwekezaji kuwa rahisi huku matumizi ya intaneti yakiweka urahisi kufanikisha suala hilo.

“Lakini hata kwa wasiokuwa na simu kubwa wanaweza kuwekeza, hii inafanyika ili kugusa makundi yote ya wawekezaji wadogo na wakubwa ili kuweza kufikia fursa hizi na mwaka ujao tutafanya zaidi ili watu wengi zaidi wafikiwe,” amesema.

Amesema maboresho ya teknolojia yanayofanyika yanalenga kuendana na mabadiliko yanayoshuhudiwa duniani ili uwe wa kisasa utakaowezesha na walio nje ya Tanzania kuwekeza kama waliopo Tanzania.

“Lengo letu ni kuunganisha na benki zote hata za kimataifa na mwekezaji akiwa nchi yoyote mfumo uwe umeunganishwa kwenye mifumo yote ya usafirishaji fedha,” amesema.

Akielezea kwa nini watu wawekeze, Simon amesema mifuko hiyo ni njia nzuri ya ujumuishaji wa kifedha wa wananchi wote, zamani mtu alikuwa akifanya biashara bila kuweka fedha sehemu inayotakiwa.

“Ilikuwa ngumu kuweka fedha kwenye mfumo rasmi,  wengine walichimbia ardhini na ilikuwa nje ya mzunguko wa uchumi, lakini sasa tutaipata itaingia kwenye mfuko tutawekeza katika benki na kampuni zinazofanya uzalishaji hivyo mzunguko unakuwa mkubwa,” amesema.

Akieleza kwa nini ni muhimu vijana kutumia fursa hiyo amesema inawapa uhakika wa fedha zao kuendelea kuzalisha wakati wakiendelea kutimiza ndoto zao.

“Kijana anakuwa na muda mrefu wa kuwekeza kwa ajili ya kuendesha maisha huku mtaji wake unakua bila kujali ni kiwango gani cha fedha wamewekeza.

“Unavyoongeza na sisi tunakuongezea faida na mwisho wa siku kile ulichotaka kukifanya unakifanya hata kama kuagiza IST,” amesema Simon.

Mwenyekiti wa Bodi wa UTT Amis, Profesa Faustine Kamuzora amesema wamejipanga kuendelea kuleta mazao mbalimbali yatakayowezesha watu kuwekeza jambo litakalochochea ufikiaji wa uchumi wa Dola 1 trilioni  za Marekani mwaka 2050.

“Uwekezaji sekta ya fedha ni muhimu, unawawezesha kuwekeza katika kiwango kidogo na kuwapatia faida ambayo inaweza kuongezeka na kujenga uchumi,” amesema.