Dar es Salaam. Mwaka 2025 unaisha kwa kushuhudia mageuzi makubwa katika nyadhifa za juu serikalini na ndani ya vyama vya siasa nchini, hali inayoashiria mwelekeo mpya wa uongozi na utendaji kwa mwaka 2026.
Hatua hiyo, pamoja na kuibua matumaini mapya kwa wananchi na wafuasi wa vyama, imeambatana pia na mijadala kutokana na baadhi ya viongozi kuachia nafasi zao ghafla kiasi cha kuacha gumzo miongoni mwa jamii.
Miongoni mwa matukio yaliyoibua mjadala ni uamuzi wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kutangaza kutogombea ubunge wa Ruangwa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) siku ya mwisho ya kuchukua fomu, licha ya awali kueleza nia ya kugombea.
Vilevile, aliyekuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Uyole, Dk Tulia Ackson, aliyechukua fomu ya kutetea nafasi hiyo, lakini alijitoa dakika za mwisho bila kutoa sababu, hatua iliyozua mshangao miongoni mwa wanachama na wananchi.
Kwa upande mwingine, aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, alimuandikia barua Rais Samia Suluhu Hassan kuomba kupumzika. Tangazo hilo lililotolewa hadharani na Rais lilikuwa mara ya kwanza kuwahi kutokea nchini, huku uamuzi huo ukiacha maswali na mitazamo tofauti.
Hata hivyo, mabadiliko hayo yanatafsiriwa kama ishara ya vitendo ya sura na mwelekeo mpya wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha maendeleo, ufanisi wa utendaji kazi na ustawi wa wananchi.
Katika mwaka huu, Taifa limepata viongozi wapya katika nyadhifa nyeti za kikatiba na kiserikali, sasa ina Makamu wa Rais ni Dk Emmanuel Nchimbi, pamoja na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, wanaotarajiwa kuimarisha utekelezaji wa sera na mipango ya maendeleo ya Taifa.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia limepata Spika mpya, Mussa Zungu, na Naibu Spika wake, Daniel Sillo, wanaotarajiwa kuendeleza misingi ya demokrasia, uwazi na uwajibikaji katika mhimili wa kutunga sheria.
Katika mhimili wa Mahakama, mwaka 2025 umeandika historia kwa kumpata Jaji Mkuu wa saba wa Tanzania, George Masaju, aliyerithi nafasi hiyo kutoka kwa Profesa Ibrahim Juma aliyestaafu.
Kustaafu kwa Profesa Juma kulikuja baada ya kuongezewa muda wa utumishi, suala lililowahi kuibua mijadala miongoni mwa wadau wa sekta ya sheria.
Aidha, kuanzishwa kwa Wizara mpya ya Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, na uteuzi wa Joel Nanauka kuwa waziri wake, kunatafsiriwa kama dhamira ya Serikali kushughulikia kwa kina masuala ya vijana na ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.
Katika medani ya vyama vya siasa, CCM na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) navyo vimepata viongozi wapya wa kiutendaji. Dk Asha-Rose Migiro ameteuliwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia, kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, akirithi nafasi ya Nchimbi, ambaye sasa ni Makamu wa Rais.
Kwa upande wa Chaumma, Salum Mwalimu amechaguliwa kuwa Katibu Mkuu mpya, akirithi nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Mohamed Masoud.
Mabadiliko haya kwa ujumla yanaendelea kuacha alama ya sura mpya ya uongozi wa kisiasa na kiserikali nchini, huku jamii ikiendelea kufuatilia kwa karibu mustakabali wa mwelekeo huo.
Tathmini ya wadau na maoni yao
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini, Hamduny Marcel, amesema baadhi ya viongozi walioacha au kutoendelea na nafasi zao waliibua mjadala mkubwa kutokana na mchango wao mkubwa na uwajibikaji uliokuwa unaonekana wazi kwa wananchi, licha ya kuwepo kwa sababu za msingi zilizopelekea maamuzi hayo.
Akitoa mfano wa aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk Mpango, Marcel amesema kuwa nia ya kuachia ngazi ilianza tangu awamu ya tano kutokana na changamoto za kiafya. Hata hivyo, hatua hiyo ilisababisha mjadala mpana kwa sababu wananchi wengi walimpenda na walithamini utendaji wake.
“Dk Mpango alifanya kazi kwa uadilifu, hekima, nidhamu na weledi mkubwa. Sifa hizo ndizo zilizowaumiza wengi na kusababisha mijadala mikubwa,” amesema Marcel.
Kuhusu aliyekuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Marcel amesema ilitarajiwa asigombee tena nafasi ya ubunge, akieleza kuwa kutoka kuwa mtendaji mkuu wa shughuli za Serikali na baadaye kuwa mbunge wa kawaida kunge leta hoja za kiitifaki na kuvunja heshima ya nafasi aliyowahi kushika.
“Alikuwa mbunge kwa muda wa kutosha, na kugombea tena kungesemekana kama uroho wa madaraka. Inawezekana pia kulikuwa na sababu nyingine zisizo wazi ili abakie na heshima yake na aendelee kuitumikia nchi kwa nafasi nyingine,” amesema.
Kwa upande wa Dk Tulia, Marcel amesema hatua yake ya kutoendelea ilishangaza wengi kutokana na umri wake mdogo na uwezo mkubwa aliouonesha katika kuongoza shughuli za Bunge.
“Aliacha ghafla na ameacha kumbukumbu ya kipekee. Inawezekana kulikuwa na mambo ya ndani ambayo wananchi hawawezi kuyaelewa, hasa ikizingatiwa kuwa alishinda kwa kura nyingi,” amesema.
Akizungumzia Jaji Mkuu Masaju, Marcel amesema mabadiliko hayo hayakushangaza kwa kuwa yalitokana na ukomo wa muda wa kikatiba wa aliyekuwa madarakani.
Kuhusu kuibuka kwa sura mpya serikalini na ndani ya vyama vya siasa, Marcel amesema mabadiliko hayo yanaakisi mageuzi na maandalizi ya viongozi wengi kupitia mifumo sahihi ya uongozi.
Akitolea mfano wa Dk Nchimbi, amesema amepitia makuzi ya kisiasa tangu akiwa kijana, akishika nyadhifa mbalimbali za uwaziri hadi ubalozi, na sasa anatarajiwa kupimwa kwa matokeo ya utendaji wake.
“CCM tangu zamani ilikuwa na utaratibu wa kuandaa viongozi, ingawa kulikuwa na nyakati ambazo maandalizi hayo hayakuonekana wazi,” amesema.
Pia amesema hata kwa Waziri wa Vijana, Joel, mafanikio yake yametokana na kupitia ngazi zinazokubalika za uongozi.
“Jambo muhimu katika kupata viongozi bora ni kuzingatia mifumo sahihi ya maandalizi, ikiwemo kupitia ngazi za vijana au shule za uongozi, ili waweze kusikiliza na kutatua kero za wananchi kwa ufanisi,” amesema Marcel.
