Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza, amesema hivi sasa KKKT haisemwi vizuri kutokana na kupoteza ushuhuda wa kimatengenezo.
Amesema hakuna dhambi wanaikemea ambayo haitendwi ndani ya kanisa hilo, akihoji kama haipo itajwe.
Mwananchi imemtafuta Mkuu wa KKKT, Askofu Alex Malasusa ambaye ndiye msemaji wa kanisa hilo kuzungumzia kauli hiyo lakini simu yake haikuwa ikipatikana.
Askofu Bagonza ametoa kauli hiyo katika ibada ya ubarikio wa wachungaji Dayosisi ya Karagwe Usharika wa Lukajange- Kanisa Kuu leo Desemba 21, 2025
“Hivi sasa KKKT haisemwi vizuri kutokana na kupoteza ushuhuda wa kimatengenezo. Hakuna dhambi tunayoikemea ndani ya kanisa ambayo hatuitendi wenyewe ndani ya kanisa, haipo, ipi itaje, unataka kuniambia hakuna rushwa ndani ya kanisa, nyie hamsubiri kupokea rushwa mnadokoa hadi sadaka,”amesema.
Askofu Bagonza ameongeza kuwa “Ubadhilifu wa mali ndani ya kanisa, miradi inakufa watu wakiona, ulevi, hamnywi …..?wangapi hawanywi…..?, ufisadi, uzinzi tumebaki kushughulikiana wenyewe kwa wenyewe badala ya dhambi,”amesema.
Askofu Bagonza amesema katika utumishi wake akiwa mchungaji kwa miaka 33 sasa, miaka 23 ametumika kama askofu na alipoanza huduma wakati huo watu walikuwa wakiogopa kusema uongo kwa hofu kwamba mtu akisema uongo atakufa.
Kwa sasa amesema ipo hofu ya kusema ukweli lakini Mungu hajabadilika isipokuwa binadamu ndio wamebadilika.
“Ni yeye yuleyule jana, leo na siku zote ndiye njia ya kweli na uzima, hawezi kutumikiwa na mchungaji muongo muongo au askofu tapeli tapeli hawezi, inampasa mtumishi wa Mungu kuwa mtumwa na mfungwa wa kweli, bosi wa kwanza wa mchungaji anaitwa bwana ukweli,”amesema.
Akitoa ujumbe kwa wachungaji wapya, Askofu Bagonza amesema kanisa lililofuata baada ya mitume kuuawa, ibada ya ubarikio ilikuwa ya machozi na maombolezo na hapakuwa na sherehe wala vigelegele.
“Daraja la uchungaji haikuwa fahari yeyote zaidi ya mateso na utii usiokuwa na mipaka, kuukubali uchungaji ilikuwa ni sawa na kuitwa gaidi au uhaini kwa nyakati zetu mbele ya kanisa na mbele ya Serikali ya Kirumi ya wakati ule,”amesema.
Askofu Bagonza amesema utume walioitiwa viongozi hao umejaa machozi, mateso ya mitume ya wakati ule na sasa yanafanana.
Ametaja aina tatu za mateso zitakazowapata wachungaji hao endapo watasimama katika zamu zao, “Kwanza mtateswa na kanisa lenu, mitume waliteswa ndani ya sinagogi hata nyie mkisimamia kweli mtateswa na kanisa lenu kabla ya kuteswa na dunia.
“Juzi hapa nilimsikia Askofu mmoja tena anayeheshimika hapa nchini akionya wachungaji wake na maaskofu wenzake wakae kimya kwa sababu hali ni mbali akisema hata kimya ni jibu.”
Sasa mimi nawaonya msikae kimya, msiwafuate maaskofu wa namna hiyo hata ikiwa ni mimi, mchungaji anayefanya kazi yake vizuri ajiandae kuteswa na kanisa lake,”amesema.
Mateso ya pili aliyotaja Askofu Bagonza ni kutoka kwa Serikali, akifafanua hilo wakati wa Yesu Kristo Serikali iliwatesa Wakristo na mitume kwa sababu hawakupenda kutii Serikali dhalimu ya kikoloni kutoka Rumi.
Amesema siku hizi Serikali zinaongozwa na waumini wao ndio maana hakuna mateso.
“Hakuna Serikali yeyote duniani inayovumilia unabii haipo, iwe ya kweli au wa mchongo kama tunaouona siku hizi kwa hiyo jiandaeni kuteseka, kuzushiwa na kudhalilishwa,”amesema
Aina nyingine ya mateso aliyoyataja Askofu Bagonza ni ya familia akisisitiza hakuna nabii anayekubalika kwao, watainuka watu ndani ya familia kupinga utume.
Watu aliowatolea mfano huenda wakampinga nabii kwao ni mke, ndugu, mtoto na wengineo.
Akinukuu Zaburi 105, Askofu Bagonza amesema msiwaguse masihi wangu wala msiwadhulumu, haikuwazuia wafalme wabaya, haikuwazuia wanafamilia wabaya kuwagusa wateule wa Mungu,”amesema.
Amewataka wateule hao wa Mungu kujilinda nafasi zao Kristo asikataliwe kwa sababu yao bali kwa ukaidi wa watu wanaowahudumia.
Askofu Bagonza aliwataja wachungaji waliobarikiwa ni Mchungaji Essau Erasto, Baraka Shubira, Lightness Simon, Vennita Nyango, Julius Baltimayo.
