GULAM DEWJI AIPONGEZA TRA KWA KUPAMBANA NA MAGENDO

:::::::::

Mfanyabiashara maarufu nchini na mmiliki wa Kiwanda cha East Coast Oils and Fats Limited kilichopo jijini Dar es Salaam ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa jitihada inazofanya katika kupambana na uingizwaji wa mafuta ya kupikia ya magendo.

Hatua hiyo imekuja baada ya Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda kufanya ziara ya kutembelea Viwanda vya mafuta jijini Dar es Salaam tarehe 20.12.2025 ikiwa ni sehemu ya kutafuta suluhisho la kupambana na uingizwaji wa mafuta ya kupikia kwa njia za magendo nchini.

Dewji amesema uingizwaji wa mafuta hayo ya magendo haukubaliki kwani unaharibu biashara na kudhoofisha viwanda vya ndani kauli ambayo iliungwa mkono na uongozi wa viwanda vingine kikiwemo kiwanda cha Mikoani Traders, Bw. Saleh Afif Mkurugenzi wa Utawala ambaye amesema vita dhidi ya Magendo si ya TRA peke yake bali ni ya wananchi wote.


Akizungumza wakati wa ziara hiyo Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema lengo la ziara yake ni kutafuta suluhisho la kudumu la kupambana na uingizwaji wa mafuta ya kupikia ya magendo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wamiliki wa Viwanda vya mafuta ya kupikia na waingizaji wa mafuta nchini.

Amesema miongoni mwa hatua za kupambana na magendo anaunda timu ya wataalam itakayohusisha wauzaji wa mafuta, waingizaji wa mafuta na wamiliki wa viwanda vya mafuta ya kupikia ili kupata maoni ya kila upande.

Amesema TRA haizuii kuingizwa mafuta nchini maana mafuta yanayozalishwa hayakidhi mahitaji ya nchi lakini kinachotakiwa ni kufuata utaratibu wa kuingiza mafuta hayo.