Lishe sahihi ina mchango mkubwa katika kulinda na kuboresha afya ya figo. Kwa mujibu wa wataalamu wa lishe, uchaguzi wa matunda sahihi unaweza kusaidia kupunguza mzigo kwa figo, hasa kwa watu wenye matatizo ya figo au wanaoishi na ugonjwa wa figo sugu (CKD).
Akizungumza kuhusu umuhimu wa lishe, Dkt. Dao Thi Yen Thuy, Mkuu wa Idara ya Lishe na Dietetics katika Hospitali ya Tam Anh, Ho Chi Minh City, anasema wagonjwa wa figo wanapaswa kudhibiti kwa makini ulaji wa potasiamu, sodiamu na fosforasi, kwani madini haya yakizidi huongeza kazi nzito kwa figo. Aidha, anashauri kula matunda yenye antioxidants na nyuzinyuzi (fiber) kwa wingi.

Haya hapa ni matunda matano yanayosaidia afya ya figo:
1. Tufaa (Apples)
Tufaa halina sodiamu na lina kiasi kidogo cha potasiamu na fosforasi. Tunda hili lina nyuzinyuzi aina ya pectin ambazo husaidia kupunguza cholesterol, kudhibiti sukari kwenye damu na kulinda figo dhidi ya hatari zinazotokana na magonjwa ya moyo na kisukari.
2. Blueberries
Blueberries yana vitamini C, nyuzinyuzi na antioxidants aina ya anthocyanins zinazosaidia kulinda seli za figo dhidi ya uharibifu. Pia yana kiwango kidogo cha potasiamu na fosforasi, hivyo yanafaa kwa watu wenye matatizo ya figo.
3. Strawberries
Strawberries ni chanzo kizuri cha vitamini C, manganese na antioxidants ambazo hupunguza uvimbe mwilini na kuimarisha kinga ya mwili. Kiwango chake cha madini hatarishi kwa figo ni kidogo, jambo linaloyafanya yawe salama kwa afya ya figo.
4. Cherries
Cherries yana kemikali asilia na antioxidants zinazosaidia kupunguza uvimbe na kulinda seli za mwili. Kwa kuwa yana kiwango cha chini cha potasiamu, sodiamu na fosforasi, cherries ni chaguo zuri kwa wagonjwa wa figo.
5. Pears
Pears ni matunda laini, yenye maji mengi na rahisi kumeng’enywa. Yana potasiamu kidogo na yana nyuzinyuzi, vitamini C na antioxidants zinazosaidia mmeng’enyo wa chakula, afya ya moyo na kulinda seli za figo.
Ushauri wa Daktari
Dkt. Thuy anashauri wagonjwa wa figo:
-
Kuepuka au kupunguza matunda yenye potasiamu nyingi kama ndizi, machungwa, maembe yaliyoiva, parachichi na viazi vitamu
-
Kupunguza matumizi ya chumvi na viungo vikali
-
Kuepuka vyakula vya viwandani na vyenye chumvi nyingi
-
Kugawa chakula katika milo midogo midogo ili kupunguza mzigo kwa figo
Pia, wagonjwa wanashauriwa kunywa maji kwa kiwango kinachopendekezwa na daktari kulingana na hali yao ya afya, kwani maji mengi au machache kupita kiasi yanaweza kuathiri figo.
