Mbinu za ulinzi faragha ya familia zama za dijitali

Dar es Salaam. Kadiri teknolojia inavyozidi kuingia katika maisha ya kila siku, suala la kulinda faragha ya familia limekuwa muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Mitandao ya kijamii, vifaa vya kisasa na mifumo ya kidijitali imeleta urahisi mkubwa, lakini pia imefungua mianya mipya ya uvunjifu wa faragha kwa watu wa rika na mazingira mbalimbali.

Wataalamu wa usalama wa mtandaoni wanahoji kuwa, katika enzi ya sasa, kila kaya inahitaji kuchukua hatua madhubuti ili kujilinda dhidi ya hatari zinazoongezeka.

Kwa mujibu wa wataalamu, tatizo la ufunuaji wa taarifa binafsi si la watu maarufu pekee. 

Familia za kawaida pia ziko hatarini kupitia taarifa wanazochapisha bila kujua kama vile kuweka  picha zinazoonyesha maeneo ya nyumba, watoto au taarifa za safari kwa familia.

Mara nyingi, taarifa hizi hutumiwa na wahalifu wanaofuatilia mienendo ya watu kupitia mtandao. Kwa sababu hiyo, ushauri wa kwanza unatolewa kwa familia zote ni kupunguza kiwango cha taarifa binafsi zinazoonekana hadharani , ambazo watu wengine hupitiliza kwa kuweka hata taarifa za ndani za kifamilia mtandaoni. 

Katika upande wa usalama wa kidijitali, wataalamu wanasisitiza umuhimu wa kutumia nywila imara  katika akaunti zote muhimu. 

Hii ni kutokana na ukweli kwamba mashambulizi ya mitandaoni yanayojulikana kama “hacking”yameongezeka na hayalengi tena mashirika makubwa pekee. 

Kaya ambazo hazijasasisha vifaa au programu zao, au zinazotumia nywila dhaifu, hujikuta katika hatari ya kuingiliwa na wahalifu wa kidijitali.

Picha na video zinazopakiwa mitandaoni pia zimekuwa chanzo kikubwa cha uvunjifu wa faragha.

 Pamoja na familia nyingi kutokuwa na nia mbaya kuandika picha hizo na hata maelezo yake,  bado hali hiyo huweza kutoa taarifa ambazo zinaweza kutumiwa vibaya.

 Wataalamu wanashauri kuficha au kupunguza sehemu za nyuma kwenye picha, au kuhakikisha kuwa washiriki wote wanatoa ridhaa kabla ya picha zao kusambazwa mtandaoni.

Hatua za kulinda faragha ya familia pia zinahusu taarifa za makazi.

Kwa sasa, huduma nyingi za mtandaoni hukusanya na kuchapisha taarifa za watu bila wao kujua.

Familia zinashauriwa kuangalia na kuomba kuondolewa kwa taarifa zao katika baadhi ya hifadhidata hizi. 

Watoto wanapewa uzito wa pekee katika masuala ya faragha. Kwa kuwa wao ndiyo hutumia mitandao ya kijamii na michezo ya mtandaoni kwa kiwango kikubwa, wana hatari zaidi ya kuingilika au kushawishiwa. 

Wazazi wanashauri kutoa elimu ya mara kwa mara kuhusu matumizi salama ya mtandao, umuhimu wa kutoshiriki taarifa binafsi na hatari ya kuwasiliana na watu wasiojulikana.

Japo  shule zinaweza kutoa elimu kuhusu  dijitali, lakini jukumu kubwa lipo mikononi mwa wazazi.

Kwa upande wa watu maarufu, kama vile wanamichezo, wasanii au viongozi wa kisiasa, suala la faragha ni nyeti zaidi kutokana na umakini mkubwa wanaopata kutoka kwa umma na vyombo vya habari. 

Wengi wao wamekuwa wakitumia mikakati ya kuepusha familia zao kuonekana hadharani, ikiwemo kutumia akaunti  binafsi au kuratibu taarifa kupitia wasimamizi. 

Hata hivyo, wataalamu wanasema kuwa kanuni hizo zinafaa kutumiwa na familia yoyote, kwani zinweka mipaka kati ya maisha ya umma na yale ya nyumbani.

Sheria za kulinda taarifa binafsi zimeanza kuimarishwa katika nchi mbalimbali, na watu wana haki ya kuomba kuondolewa kwa taarifa binafsi mtandaoni au kuchukua hatua za kisheria pale wanaponyanyaswa, kufuatiliwa au kufichuliwa bila ridhaa. Familia zinashauriwa kujua haki zao na kutafuta ushauri wa kisheria inapohitajika.

Wataalamu wanasisitiza umuhimu wa busara katika kushirikisha taarifa. Mara nyingi, uvujaji wa taarifa hutokea kupitia watu wanaoaminika kama marafiki, majirani au wanachama wa makundi ya mtandaoni. 

Uamuzi wa kushirikisha au kutoshirikisha taarifa unapaswa kufanywa kwa umakini, kwa kutanguliza usalama wa familia.

Katika ulimwengu unaoendelea kuunganishwa kupitia mtandao, faragha inabaki kuwa nguzo muhimu ya usalama. 

Familia zinahimizwa kuchukua hatua zinazowezekana leo ili kulinda amani ya kesho.

Kwa kufanya hivyo, zinaweza kuhakikisha kuwa mambo yao binafsi yanabaki mahali yanapostahili: ndani ya mipaka yao na kwa usalama.