MEYA wa Jiji la Dar es Salaam Nurdin Bilal ‘Shetta’, amesema milango ya ofisi yake iko wazi kwa wasanii na wanamichezo kwa jambo lolote linaliweza kusukuma mbele tasnia hiyo.
Aidha amesema, anakusudia kuanzisha timu maalumu ya Jiji la Dar es Salaam na kuiwezesha kucheza ligi mbalimbali ikiwemo Ligi Kuu Tanzania Bara ukiwa ni mkakati wa kuinua vipaji vya soko.
Pia, amesema anakusudia kuanzisha Bao la Meya wa Jiji la Dar es Salaam kwa timu za soka Wilaya ya Ilala ikiwa ni kuunga mkono jiti hada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuinua sekta ya michezo.
Ameyasema hayo jijini Dar es Salaam alipofungua Bonanza la kumuenzi mdau wa soka Tarafa ya Kariakoo, Mudrick Rashid ‘Mud Bonge’ lililofanyika katika vianja vya Mnazi Mmoja.
“Nimehudumu katika muziki kwa miaka 15. Muziki, sanaa michezo ni kitu kimoja.Katika uongozi wangu wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam niwatoe mashaka, chochote mnacho kiona kinaweza kusogeza tasnia mbele basi ofisi yangu iko wazi,”alisema.
Ameeleza ataangalia uwezekano wa lutengeneza timu ya soka ya Jiji la Dar es Salaam ambayo itafika hadi Ligi Kuu.
“Tutaongea na wadau kuhakikisha tunasapoti vipaji.Ilala ndiyo jiji linaloongoza nchi nzima kwa mapato, hivyo tunataka kuongoza hata katika michezo,”amesema Shetta.
Amepongeza waandaji wa bonanza hilo la kumwenzi mdau huyo huku akitoa wito wa uanzishaji wa vituo vya kuinua vipaji vya wachezaji wakiwa bado wadogo.
“Tunapomuenzi mdau huyu basi tukumbuke kuanzishe vituo vya kulea vipaji kama wenzetu,”amesema meya huyo.
Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa Maalumu wa Ilala (IDFA) Kondo Mussa, alimshukuru Shetta kwa ahadi hizo na kueleza uongozi wake utaongeza chachu kwa michezo na wanamichezo jijini Dar es Salaam.
“Tunafarijika na kauli hii ya Meya kufungua milango kwa wadau wa michezo na sanaa. Ili tasnia ikue inahitaji wadau. Tunaona mpira wa Ilala sasa unakwenda kubadilika kwani kiongozi ameonesha nia,”amesema.
Mratibu wa wa bonanza hilo Katibu wa Veterani Kariakoo, Mwinyi Mudete, amesema lilishirikisha veterani mbalimbali katika kumuenzi mdau Mudi Bonge.
“Mudi Bonge alikuwa na mchango mkubwa katika soka hapa nchini hasa kwa wachezaji wa akiongoza rimu ya Kibasila iliyokuwa na makao makuu yake Kata ya Gerezani. Amewatoa wanamichezo kama Credo Mwaipopo, Said Swed, Salumu Swed, Hussein Swed, Kipanya Malapa na John Mwansasu,”mesema Mwinyi.


